Sunday, October 31, 2010

RAIA WA TANZANIA WAANAENDELEA NA ZOEZI LA UPIGAJI KURA

Tanzania LEO

Raia wa Tanzania wameanza kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa leo.

Kuna ushindani mkali katika kinyanganyiro cha kuwania kiti cha urais.

Miongoni mwa watu wanaowania kiti hicho ni pamoja na rais wa sasa Jakaya Kikwete, ambaye alizoa asilimia 85 ya kura zote zilizopigwa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Wakosoaji wa Rais Kikwete wanasema ameshindwa kukabiliana na ufisadi na kuhakikisha kuwa rasilimali ya nchi inawafikia raia wa kawaida.

Rais Kikwete anapambana na wapinzani wengine akiwemo Willibrod Slaa, ambaye ameahaidi kupambana na ufisadi na kuanzisha huduma za afya na elimu bila malipo nchini humo endapo atachaguliwa kuongoza taifa hilo.

Mwingine ni Ibrahim Lipumba ambaye amehaidi kubuni serikali ya muungano wa kitaifa ili kutatua matatizo ya taifa ikiwa atashinda uchaguzi huo.

Wapiga kura milioni 19.6 wanatarajiwa kushiriki katika zoezi hilo.

Mwandishi wa BBC Kisiwani Zanzibar anasema matatizo kadhaa yameanza kujitokeza katika majimbo kadhaa.

Anasema kura za kuwachagua wabunge hazikutokea na hivyo kuwalazimisha kukosa kuwachagua wabunge wao.

Licha ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha kisiwani Pemba idadi kubwa ya wapiga kura wanaendelea kujitokeza

Saturday, October 30, 2010

WAZIRI MKUU MIZENGO PETER PINDA NJOMBE.

WAZIRI MKUU MIZENGO PETER PINDA.

Waziri mkuu na Mjumbe wa kamati kuu ya siasa ya chama cha mapinduzi ccm,na mbunge wa jimbo la mpanda mheshimiwa , mizengo pinda,amefanya ziara mkoani hapa na ameupongeza uamzi wa serikali wa kuugawa mkoa wa iringa katika mikoa miwili ya njombe na iringa.

Waziri pinda ameyasema hayo wakati akiwahutubia wananchi wa jimbo la njombe kaskazini katika ziara yake ya kufunga harakati za kampaini za chama cha mapinduzi kwa majimbo ya njombe.

Akiwa katika jimbo la njombe kaskazini katika ziara yake ya kwanza mkoani hapa pinda amewapongeza viongozi wa mkoa wa iringa katika juhudi za kuboresha sekta ya elimu.

Katika sekta ya elimu mheshimiwa pinda ambae pia ni waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa tanzania amewapongeza viongozi wa mkoa wa iringa kwa ujenzi wa vyuo vikuu ambapo sasa vimefikia 6.

Pia kufuatia kujengwa kwa kituo kikubwa cha afya katika mji wa makambako Waziri Pinda amehaidi kutoa gari la wagonjwa katika mji huo wa makambako.

Katika hatua nyingine waziri pinda amewataka wananchi mkoani hapa kujitokeza katika kupiga kura ili kuwachagua rais, wabunge na madiwani.

Friday, October 29, 2010

UJIO WA PILI DOKTA SLAA NJOMBE



Mgombea Urais kwa tikeki ya chama cha demokrasia na maendeleo Chadema dokta WILBROD SLAA leo amefanya ziara yake mkoani njombe katika maeneo ya Saja, Ilembula na Kata ya Igwachanya kwa lengo la kuzinadi sela za chama hicho.

Dr.Slaa ambaye tayari alishafanya mikutano yake ya kampeni katika mkoa wa njombe safari hii amekuja ikiwa ni siku chache kufikia siku ya uchaguzi hapo jumapili.

Akiwa katika kata ya saja ambapo helkopta anayotumia mgombea huyo ilishindwa kutua kwa muda kutokana na hali mbaya ya hewa katika eneo hilo lakini nusu saa baadae helikopta hiyo iliweza kutua katika eneo hilo.

Akiwahutubia wananchi wa maeneo hayo ya saja na ingwachanya nakuzinadi sera za chama hicho DOKTA WILBROAD SLAA amewaomba wananchi hao kukichagua chama cha chadema ili kuweza kuleta mabadiliko nchini.

mgombea huyo wa urais pia amehaidi kuimarisha elimu ya mtanzania ili kupiga vita ujinga, umasikini na maradhi,na kwamba ili kuboresha elimu nchini si kuishia elimu ya msingi bali ni hadi vyuo, kwani elimu ya lazima kwa mtoto wa kitanzania si tu elimu ya msingi.

Mara baada ya kumaliza mkutano katika eneo hilo la igwachanya dokta Slaa ataelekea katika mkoa wa Ruvuma katika eneo la mbamba bay wilayani Mbinga na baadae katika wilaya ya Songea akiendelea na kampeni zake katika mkoa huo.




Wakati Mkoa wa Iringa ukiwa bado unashikilia nafasi ya kwanza kitaifa kwa kuwa na kasi kubwa ya maambukizi ya ukimwi, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Manispaa ya Iringa (Iruwasa), imeanza mkakati wa kutenga Sh 4 milioni kila mwaka kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo kwa wafanyakazi wake.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa baraza la wafanyakazi wa Iruwasa na bodi mpya ya mamlaka hiyo, Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Marko Mfugale alisema wameamua kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba, ukimwi ni kati ya magonjwa ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma utendaji wa kazi, kutokana na kuathiri wafanyakazi wengi.

Alisema mamlaka hiyo imekuwa ikiendesha semina na mafunzo mbalimbali kazini kwa ajili ya kutoa elimu ya ukimwi kwa wafanyakazi wake, sambamba na kuwatumia washauri nasaha kwa ajili ya kuwapima kwa hiari wafanyakazi hao.

“Ukimwi unaathiri kila kona, na umekuwa ukipoteza nguvu kazi kubwa ya taifa, tumeona ni muhimu kwetu kuanza kupambana na janga hili kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi kwani hakuna ambaye hajawahi kuathiriwa na ugonjwa huu tishio,” alisema Mfugale.

Katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi na kuongeza ufanisi kazini, Mfugale alisema kwa kushirikiana na Benki za CRDB na Barclays wamefanikiwa kuwakopesha wafanyakazi zaidi ya Sh 333.2 milioni sambamba na kuanzisha chama cha akiba na mikopo.

“Watumishi wetu wamekuwa wakipata mikopo kutoka maeneo mbalimbali na mamlaka inahakikisha wanapata stahili zao ili kuleta ufanisi kazini kwani kama wakiwa na kipato duni, ni vigumu sana kuendeleza jitihada za kutoa huduma bora za maji kwa jamii,” alisema.

Awali, Mwenyekiti mpya wa bodi ya Iruwasa, Cecilia Shirima aliitaka bodi hiyo kufanya kazi vizuri na kufikia malengo ya kufikisha huduma ya maji safi na majitaka kwa asilimia 100 na kupata alama ya kiwango cha ubora cha utoaji huduma kimaifa (ISO) kama ilivyo kwa mamlaka nyingine.

Bodi hiyo inaundwa na wajumbe wengine, Katibu tawala Mkoa wa Iringa Getrude Mpaka, Katibu wa CCM, Mkoa wa Iringa, Mary Tesha, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mkwawa, Profesa Mushi na Mwanasheria Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Reuben Swai.