Sunday, July 30, 2017

ZAIDI YA WAFANYAKAZI 400 MKOANI MOROGORO HATIANI KUFUTWA KAZI

Zaidi ya Wafanyakazi 400 wa Serikali wanatarajia kuondolewa kazini mkoani Morogoro kutokana na kushindwa kujiendeleza kielimu baada ya kuajiriwa miaka 13 iliyopita wakiwa na vyeti vya elimu ya msingi.
Watumishi hao ambao wengi wao ni wauguzi, wahudumu wa afya, madereva, wahudumu wa ofisi, watendaji wa mitaa, vijiji na kata tayari wamenyimwa mishahara yao ya mwezi huu.
Akizungumzia zoezi hilo aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Kimamba wilayani Kilosa, Mashaka Motile amesema katika wilaya hiyo watumishi zaidi ya 80 wamenyimwa mshahara bila maelezo yoyote na walipofuatilia ndipo walipofahamishwa kuwa walipewa muda wa kujiendeleza na wameshindwa kufanya hivyo.
“Hakuna barua yoyote tuliyopewa ya kusimamishwa kazi ila mshahara wa Julai hatujapewa na tulipofuatilia tuliambiwa kuna waraka wa Serikali unaosema wale wote walioajiriwa kuanzia mwezi Mei 20, 2004 wakiwa na elimu ya msingi na wameshindwa kujiendeleza wanatakiwa kuondolewa,” amesema.
Motile anasema yeye na baadhi ya watendaji wengine walisimamishwa kazi kimakosa kwani agizo linasema wasimamishwe kazi walioajiriwa kuanzia Mei 20, 2004 lakini wao waliajiriwa Mei Mosi, 2004.
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali, mhudumu wa afya wa manispaa ya Morogoro ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema uamuzi huo umekuwa wa ghafla mno na haujatoa muda wa wao kujiendeleza.
“Naiomba serikali ituongeze japo miaka mitatu ili tuweze kujiendeleza maana hivi tulivyosimamishwa kazi ghafla familia zetu zitaathirika sana na kuna hatari ya watoto wetu kuacha shule, tunaomba tuongezewe muda,” amesema.
Alipotakiwa kuzungumzia zoezi hilo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa, Kessy Mkambala alisema bado zoezi linaendelea litakapokamilika ndo ataweza kulizungumzia.
Naye Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) mkoani Morogoro, Lawrence Mdega amesema wamepokea malalamiko toka kwa wafanyakazi zaidi ya 150 wanaolalamika kuondolewa kwa kuwa wana elimu ya msingi.
“Nimeshawasilisha haya malalamiko makao makuu ya TALGWU ili washughulikie lakini tunachotaka watumishi hawa walipwe mshahara wa Julai ambao tayari waliufanyia kazi lakini pia walipwe mafao yao maana waliitumikia Serikali kwa uadilifu na vyeti vyao hivyo vya elimu ya msingi.

Thursday, July 27, 2017

VIONGOZI WAASWA KUSIMAMIA SERA YA ELIMU BURE ILI KUKUZA KIWANGO CHA ELIMU

Maafisa elimu kata na wenyeviti wa shule zote Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wametakiwa kuelimisha jamii juu ya tamko la Serikali la elimu bure ili wawe makini kufuatilia mienendo ya watoto pindi wawapo shuleni kwa kujenga taratibu za kuwachunguza iwapo wanafuatilia masomo yao au lah.

Wito huo umetolewa Julai 27 mwaka huu na afisa elimu Taaluma Mohamed Mwingilihela wakati wa mafunzo ya siku 3 yanayoendelea katika ukumbi wa Shule ya msingi Mazinyungu yaliyoanza Julai 25 mpaka Julai 28 kwa lengo la kutoa elimu kwa maafisa elimu kata na na viongizi mbalimbali wa shule jinsi ya kuwaelimisha wananchi wanaowazunguuka kujenga utaratibu wakuwafuatilia watoto wao pindi wawapo masomoni.

Mwingilihela amesema wanajamii wamesahau majukumu yao kwa kufuatilia masomo na mienendo ya watoto kwa kuwaacha wakizurula badala ya kukaa na kujisomea nakwenda kwenye mabanda ya video yaliyopo kila kona kwenye vijiji ambayo watumiaji wakubwa wa mabanda hayo ni wanafunzi hao.

Sambamba na hayo amewataka wazazi kuchangia michango midogo ya shule inayowahusu ikiwemo michango ya chakula cha mchana cha wanafunzi na michango mingine   ikiwemo ya miundombinu ya barabara kwani michango hiyo ipo nje na tamko ka serikali la elimu bure.

Aidha nae Mtendaji elimu kata kutoka Ulaya Wilayani Kilosa Rehema Kakwembe amesema wameyapokea kwa mtazamo chanya mafunzo hayo na watahakikisha kufikisha elimu tosha kwa jamii zote Wilayani hapa juu ya kushiriki katika michango inayowahusu hasa kufanikisha wanafunzi katika shule zote wanapata chakula cha mchana mashuleni vilevile kuwazuia watoto wao kwenda kwenye mabanda ya video na badala yake kuutumia muda huo katika kujisomea.

WAKAZI WAKILOSA WAONDOKANA NA ADHA YA USAFIRI ILIYOKUWA IKIWASUMBUA

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro imeanza kukarabati barabara zilizopo kwenye kata ya Kimamba B ili  kuwarahisishia watumiaji wa barabara hizo huduma za usafiri.
Akizungumza na Mwandishi wetu Diwani wa kata ya Kimamba B Yahaya Muhina amesema zoezi hilo limeanza kutekelezwa kwa fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kupitia makusanyo ya ndani.
Muhina amesema kwa muda mrefu barabara hizo hazikuwa nzuri kutokana na Mvua zilizonyesha na kusababisha kuharibika hivyo kukamilika kwa barabara hizo ni faraja kwa wananchi wake kwani zinawarahisishia shughuri zao.
Aidha kwa upande mwingine Diwani Muhina amewataka wananchi wa kata yake na watumiaji wengine wa barabara hizo kuzitunza ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwani Halmashauri hiyo ni kubwa na bajeti ya ukarabati wa barabara waliyonayo ni ndogo ukilinganisha na mahitaji ya vijiji na kata zinazohitaji kukarabatiwa barabara zao.
Hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imekuwa kwenye mpango wa kukarabati baadhi ya barabara za mitaa na vijiji zilizoharibika wakati wa kipindi cha mvua sehemu mbalimbali Wilayani hapa.

Wednesday, July 26, 2017

WATOTO WA JAMII YAKIFUGAJI WILAYANI KILOSAWASHINDWA KUHUDHULIA MASOMO YAO KWA AJILI YAKUCHUNGA

Jeshi  la  Polisi  Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro , Iimepiga marufuku  Wananchi  Jamii  ya Kifugaji  kuwatuma Watoto kuchunga Mifugo badala ya Kuwapeleka  Shule  kusoma.

Agizo  hilo limetolewa Julai 24 Mwaka huu na Mrakibu  Mwandamizi   wa Jeshi la Polisi (SSP)  Wilaya  ya Kilosa  Afande Mayenga  Thobiasi  Mapalala  Wakati  akizungumza  na HABARIKWANZA  Ofisini Kwake kuhusiana na Swala hilo.
Afande  Mapalala  amesema kuwa kumekuwepo na Tabia kwa Baadhi ya Wafugaji   kuwatumikisha watoto katika Kuchunga Mifugo badala ya kuwapeleka shule jambo linalowakosesha watoto hao haki yao ya msingi ya kupata Elimu ili waweze kuelimika na kuendeleza maisha yao.

Afande Mapalala  amemuomba  Afisa Elimu Msingi Wilayani  Kilosa kufatilia suala hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ili kuwabaini Wazazi na Walezi ambao wanaacha kuwasomesha Watoto , na badala  yake wanawatumikisha  katika kuchunga  Mifugo ili waweze kuchukuliwa hatua stahiki.

Aidha ametoa wito kwa jamii kutoa Taarifa kwa  Afisa  Elimu Msingi  ama Jeshi la Polisi iwapo kuna Mzazi ama Mlezi anayeacha kumpelekeka  Mtoto wake Shule na kumtumikisha katika kazi nyingine .