ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Wilbrod Slaa amejitokeza hadharani kwa
mara nyingine na kujibu watu waliojitokeza kuponda hotuba yake, aliyoitoa hivi
karibuni kuwa hawana hoja zaidi ya kumtukana.
Akizungumza kupitia kituo kimoja cha
Televisheni jijini Dar es Salaam, Dk Slaa alisema madai yote, yaliyotolewa juu
yake na baadhi ya watu wakiwemo viongozi wa Chadema na vyama vinavyounda Ukawa,
baada ya hotuba aliyoitoa, hayana msingi wowote na kwamba ni kuishiwa hoja,
ndio maana walimtukana badala ya kujibu hoja.
“Nashukuru hoja zangu zote
hawajazijibu, sasa wanapiga tu propaganda, hata Rostam Aziz alijaribu kujibu,
lakini akatukana tu kama alivyonitukana mwaka 2007 badala ya kujibu hoja na
mimi nasema ufisadi ni hoja,”
alisema Slaa.
Aidha, Dk Slaa alisema hawezi
kumpeleka mahakamani Rostam ambaye ni kada wa CCM, ambaye amemtaka Dk Slaa
ampeleke mahakamani kama anao ushahidi kuwa anaunga mkono mgombea urais kwa
tiketi ya Chadema, Edward Lowassa.
Slaa amesema yuko tayari kutoa
ushahidi wake pale Jamhuri itakapomfungulia mashitaka. “Wale ambao hawaelewi
taratibu za kesi, kuna kesi za madai ambapo mtu binafsi anafungua kesi na kesi
za jinai ambazo mtu binafsi hawezi kufungua ila Jamhuri, kesi za Jamhuri mtu
huwezi kufungua, wewe ni shahidi… mimi nikiitwa nitakwenda kutoa ushahidi dhidi
ya Rostam Aziz,” alisema Dk Slaa.
Aidha, alisema ni kweli vijana
wanataka mabadiliko na ni hoja ya msingi na pia wakulima ambao hawafaidiki na
kilimo chao, wanataka mabadiliko, vivyo hivyo kwa makundi mengine.
“Nimesema mimi Lowassa hafai,
leo, lini ameanza kuwa rafiki wa masikini?
"Lini ameanza kuwa
safi?Watanzania waache ushabiki usiofaa wapime kwa vigezo, ushabiki usio na
tija utatuangamiza,” alisema Dk Slaa, akijibu hoja
mbalimbali ambazo zimejitokeza baada ya hotuba yake hiyo, aliyoitoa mwanzoni
mwa wiki hii baada ya kutangaza kuachana na mambo ya siasa na kubaki mshauri wa
wananchi.
Akijibu shutuma dhidi yake baada ya
kutuhumiwa kutoa habari za upotoshaji juu ya maaskofu, Slaa alisema
alichokieleza siku ile anatangaza kujiengua kwenye siasa ni alichoambiwa na
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kwamba maaskofu 30
kati ya 34 walihongwa.
“Tatizo halikuwa fedha bali askofu
anaona sifa mimi kumuunga mkono mtu ambaye alitumia fedha kununua maaskofu, na
Watanzania nawaomba mtulie msikurupuke na maneno bila kuyachambua, taifa
linaangamia kwa sababu ya ushabiki usio na tija, nimeshtushwa na kauli yake,
kiongozi anayepaswa kukemea rushwa, maovu… baba askofu piga magoti Mungu wako
atazame dhamira yako,” alisema.
Dk Slaa alisema yeye ana uwezo wa
kupambanua siasa na mambo mengine na kwamba ni kweli alikutana na Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe katika Hoteli ya Serena na hiyo ni katika
kupata taarifa alizozihitaji kwa ajili ya kazi yake ya utafiti na kwamba
Mwakyembe ni chanzo cha taarifa cha kwanza na kwamba hakufanya kwa siri.
Akizungumzia picha yake ambayo
ilizunguka kwenye mitandao ya kijamii, ikimuonesha yeye akiwa na Naibu Waziri
wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
picha hiyo ni wakati wa mkutano wa vyama vya siasa na Rais wa Ujerumani,
Joachim Gauck alipokuja kwenye ziara ya kikazi Februari mwaka huu.
“Kwenye picha hizo ambazo
zinatuonesha mimi, Mwigulu na Profesa Lipumba tukimpokea Rais wa Ujerumani
alipotembelea Tanzania, leo ndio zinaletwa kuonesha eti haya ndiyo mazungumzo
ya kumng’oa Slaa, naomba niwaambie warudi nyuma waangalie hizo picha ni za lini
hazina uhusiano na mimi kujiondoa,”
alisema Dk Slaa.
Aidha, Dk Slaa alisema kuwa kuna
propaganda nyingine ambayo imetumika ambapo watu wametuma pia picha ambazo
zinamuonesha akiwa kwenye ndege, ikisemekana kwamba ametoroka nchini baada ya
hotuba, sio kweli.
Alikiri kusafiri lakini sio kwa
kutoroka, kama ambavyo imedaiwa na baadhi ya watu na kwamba amekuwa akipiga
picha na watu kwenye ndege na kwamba picha hiyo ni ya safari ambayo
alishasafiri na kurudi.
“Magazeti na mitandao wanasema Dk
Slaa hayuko nchini, lakini nadhani sasa Watanzania wanaona sasa niko hapa
studio Dar es Salaam na siko Marekani,” alisema
Dk Slaa na kuongeza kuwa uongo huo unaonesha ni aina gani za siasa zilizopo
hapa nchini.
Alisema hoja ya wapi amepata fedha
kwenda Serengeti na kuishi hotelini ni hafifu. “Nilikwenda Marekani na kukaa
kwa zaidi ya miezi 12 na kutembelea majimbo 13 na sikulipiwa na mtu yoyote
zaidi ya chama changu kulipia shilingi 500,000 kwa mshauri aliyeandaa nyaraka
ya kunisaidia katika ziara hiyo, mbona hawakuniuliza nimepata wapi fedha hizo?”