Wanachama na wafuasi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), juzi
walishambuliana kwa ngumi na silaha za jadi na kusababisha kifo cha mtu mmoja
na kujeruhi wengine watano.
Tukio hilo limetokea saa 4.09
asubuhi katika Kijiji cha Mangucha, Wilaya ya Tarime mkoani Mara wakati
wanachama na wafuasi wa vyama hivyo wakiwa kwenye shughuli za kampeni za vyama
vyao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio
hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya, Lazaro Mambosasa,
alisema chanzo cha vurugu hizo ni mapambano yaliyohusisha silaha za jadi baada
ya wafuasi wa Chadema kufanya maandamano ya kwenda kuwapokea wagombea ubunge na
udiwani waliokuwa wakitokea Kijiji cha Mwambara kwenda Kijiji cha Kegonga
ambako pia kulikuwa na mkutano wa kampeni za CCM.
Kamanda Mambosasa alisema wafuasi wa
Chadema walipofika eneo ambalo wana CCM walikuwa wakifanya mkutano wao
walinyoosha mikono juu huku wakionyesha alama ya vidole viwili ambayo huitumia
kwa salamu kitendo ambacho kiliamsha hasira za wafuasi wa CCM na ndipo
mapambano hayo yalipotokea.
Alimtaja aliyeuawa katika mapambano
hayo kuwa ni Mwita Bhoke Waite (37) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyandage
baada ya kushambuliwa na kitu chenye ncha kali kifuani na kwenye paja la mguu
wa kushoto.
Kamanda Mambosasa aliwataja
waliojeruhiwa kuwa ni Chacha Mwita Chacha (32) mkazi wa Kijiji cha Nyasage
ambaye alijeruhiwa mgongoni, mguuni na mkononi, Kimunye Chacha Mgesi (54) mkazi
wa Kegonga aliyejeruhiwa mikono yote miwili na kichwani pamoja na Elizabeth
Wiliam Marwa (43) ambaye ni mtumishi wa CCM Wilaya ya Tarime alijeruhiwa sehemu
mbalimbali za mwili kwa kupigwa na ubapa wa panga.
Majeruhi wengine aliowataja ni Oueen
Ryoba (47) ambaye ni mfanyabiashara aliyejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili
kwa kupigwa na ubapa wa panga na Nyaitati Marianya (30), mkazi wa Kegonga
aliyejeruhiwa mkononi.
Akizungumzia mwenendo wa uchunguzi
wa tukio hilo, Kamanda Mambosasa alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu
wanne wanaotuhumiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni
Kius Matiko (28) mkazi wa Kijiji cha Kegonga, Nyambari Nchagwa (43) mkazi wa
Kijiji cha Nyandage, Marwa Samweli (25) na Magasi Samweli Ghati, wote wakazi wa
Kijiji cha Kegonga Wilaya ya Tarime.
Naye Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali
ya Tarime, Rose Hosea, alipoulizwa kuhusu hali za majeruhi waliofikishwa
hospitalini hapo alisema wanne wanaendelea vizuri na matibabu isipokuwa mmoja
aliyemtaja kwa jina la Chacha Mwita Chacha ambaye amehamishiwa
Hospitali ya Musoma kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha makubwa
aliyoyapata.
Wakati huo huo, taarifa
zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni zimeeleza kuwa gari la
mgombea ubunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko limeharibiwa vibaya
katika mapambano hayo.
Alisema gari hilo lenye namba za
usajili T 282 DEE lilishambuliwa kwa mawe wakati wa mapambano hayo yakiendelea
na imekuwa vigumu kutambua mara moja waliohusika na uharibifu huo.
No comments:
Post a Comment