Tuesday, September 27, 2011

RASIMU YA HESABU KATIKA HALMASHAULI YA WILAYA YA KILOMBERO


RASIMU YA HESABU WILAYA YA KILOMBERO


Jumla shilingi bilioni 15 milioni 690 laki 944,313.00 zimepitishwa na baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya kilombero katika kikao cha kupitisha rasimu ya kitabu cha hesabu za mwisho za halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha ulioisha juni 30 mwaka huu.

Fedha hizo zimepitishwa na baraza la madiwani hii leo katika kikao maalumu cha kupitisha Rasimu ya kitabu cha hesabu za mwisho za Halmashauri kwa mwaka wa fedha ulioisha 20110/2011kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya.

Rasimu hiyo imeonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni majumuisho ya mali za kudumu ambazo zimefikia kiasi cha shilingi bilioni 10 milioni 499,16,346.00 na mali za muda mfupi shilingi bilioni 5 milioni 191 laki 927,967.00.

Aidha sehemu kubwa ya mali hizo zimetokana na fadha za ruzuku kutoka serikali kuu na michango ya wahisani kiasi cha shilingi bilioni 14 milioni 79 laki 763,492.00 na ziada ilyohifadhiwa ni shilingi bilioni 1 milioni 611 laki 180,821.00.

Friday, September 23, 2011

AFYA WA WANANCHI WA KILOSA HATARINI BAADA YA KUPASUKA KWA BOMBA LA MAFUTA,LIENDALO ZAMBIA.

BOMBA LA MAFUTA LAPASUKA WILAYANI KILOSA
Jumla ya ekari 1400 za mazao mbalimbali katika kata ya Malolo wilayani Kilosa Mkoani Morogoro,zimeharibiwa na mafuta machafu yanayovuja kutoka katika bomba kubwa linalosafirisha mafuta hayo kutoka Tanzania kwenda Zambia lililopita katika kata hiyo.

Afisa kilimo cha umwagiliaji wa kata hiyo, Bwana Mwelasi amesema bomba hilo la mafuta tangu lipasuke hadi sasa ni muda wa miezi miwili na limeharibu mfumo wa umwagiliaji wa mashamba jumla ya ekari 500 ya mazao ya vitunguu na mahindi.

Bwana Mwelasi ameyataja mazao yaliyoathirika kutokana na kupasuka kwa bomba hilo kuwa ni vitunguu na mahindi ambapo hata kiwango cha uzalishaji wa mazao hayo amesema kuwa kimeshuka.

Afisa kilimo huyo amesema mimea imekauka kutokana na mafuta yanayovuja kutoka katika bomba hilo na kuingia chini ya ardhi na kuathiri mazao na kusababisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji.

Akizungumzia uzalishaji wa mazao katika kata hiyo Amesema hapo awali kabla ya bomba hilo kupasuka ekari moja ilikuwa ikizalisha magunia 70 ya mazao, lakini sasa ekari moja inazalisha gunia 20 ya mazao kiwango ambacho amesema kimeshuka kwa kiasi kikubwa.

Hata hivyo amevitaja Vijiji vilivyoathirika na mafuta hayo kuwa ni Malolo "A", Malolo "B" na Mgogozi ambapo wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo wamo hatarini kuharibu afya zao kutokana na maji wanayotumia kwa kunywa na shughuli zinigine.

Kutokana na athari hiyo kutokea Mbunge wa jimbo la Mikumi, bwana Abdulsalam Ameri tayari amekwisha peleka mtambo wake wa kuchimba visima vya maji katika kata hiyo na kila kijiji kati ya vijiji hivyo vitachimbiwa visima viwili na kufanya idadi ya visima sita katika kata hiyo ambavyo vitasaidia kuokoa maisha ya wananchi wa kata hiyo.

UKOSEFU WA WATAALAMU MBALI MBALI KATIKA SEKTA YA KILIMO CHA MIWA NI KIKWAZO KIKUBWA KWA WAKULIMA WA MIWA KILOMBERO

UKOSEFU WA WATAALAMU MBALI MBALI TATIZO KWA WAKULIMA WA MIWA KILOMBERO
Ukosefu wa Wataalamu wa Uchumi , Mizani na Sheria ni baadhi ya changamoto zinazovikabili vyama vya Wakulima wa Miwa katika Bonde la Kilombero.

Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wetu Katibu wa Chama Cha Wakulima wa Miwa cha Msolwa Ujamaa (MUCGA) Modestus Chitemi amesema ili kuwezesha ongezeko la bei kwa Wakulima kwa Uwiano kama ilivyo kwa Nchi Jirani Wataalamu zaidi wanahitajika.

Akitolea mfano wa Nchi ya Malawi, Bwana Chitemi amesema kuwa Wakulima wa Miwa waNchi hiyo wana uwiano wa kupata asilimia Sitini (60) wakati Viwanda vya Sukari vinapata asilimia Arobaini(40).

Ameongeza kuwa kutokuwepo kwa mgao na Ruzuku ya pembejeo kutoka Serikalini katika zao la Miwa ingawa Mahitaji ya mbolea na dawa za magugu ni makubwa sana ni changamoto nyingine inayoikabili vyama vya Wakulima wa Miwa katika Bonde la
Kilombero

Mfanyakazi katika shamba la miwa akiendelea na zoezi la ukataji miwa..(picha juu)
Changamoto nyingine ni ukosefu wa Mtaji kuanzisha na kuendeleza Kilimo cha bega kwa bega na Umwagiliaji na kukosa kasi kubwa ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara na mifereji mashambani.

Mbali ya changamoto hizo katibu huyo amesema kuwa Ajira kwa Wananchi, Idadi ya Wakulima na pato la Mkulima, limeongezeka baada ya ubinafsishaji wa Viwanda na matumizi ya mfumo Mauzo ya miwa kwa uwiano wa mapato.

Shamba la miwa wilayani kilombero..

KCY YATUMIA MILIONI TISINI KWA AJILI YA MISAADA.

KCY YATUMIA MILIONI TISINI KWA AJILI YA MISAADA MBALI MBALI.

Kampuni ya Kilimo Cha Yesu (KCY) iliyopo Mpanga Wilayani Kilombero imetumia jumla ya Shilingi Milioni Tisisni (90,000,000/=) katika Mwaka 2010 kwa ajili ya Misaada mbalimbali.

Akitoa maelezo kuhusu kazi ya Kampuni ya KCY kwenye siku ya Sekta Binafsi Tanazania, Mkurugenzi wa KCY Mpanga Bruno Wicki Bruno amesema wametumia Milioni Ishirini na Laki Tano (20,500,00/=)kwa ajili ya Kusomesha watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha, Milioni Kumi na Saba na Laki Tano (17,500,000/=) misaada ya Dawa kwa walemavu na kusafirisha Wagonjwa na Milioni Kumi na Saba na Laki Tano (17,500,000/=) kusaidia Kanisa.

Shilingi Milioni Thelathini (30,000,000/=) walitumia kufidia hasara katika kampuni ya KCY na Milioni Nne na Laki sita (4,600,000/=)kwa misaada mbalimbali ya wasiojiweza.

Amesema kwa Msimu wa Kilimo uliopita walilima juml;a ya Ekari Elfu NNE mia sita(4600) na wamekopesha Shilingi Milioni Themanini (80,000,000/=) kwa Marejesho ya Riba ya Shilingi Elfu Tano(5,000) kwa Ekari kwa Vikundi kumi vyenye jumla ya Ekari elfu mbili (2000).

Kampuni ya KCY inayojishughulisha na maendeleo na kufundisha neono la Mungu kwa maneno na Matendo imeanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kusaidia Watanzania kuendelea katika shughuli za Kilimo.

TANZANIA KUNUFAIKA NA MSAADA WA EURO MILIONI 15 KUTOKA SERIKALI YA UHOLANZI

TANZANIA KUNUFAIKA NA MSAADA WA EURO MILIONI 15

TANZANIA itafaidika na msaada wa Euro milioni 15 ambazo ni sawa na (zaidi ya Sh bilioni 30 za kitanzania ) kutoka Serikali ya Uholanzi kugharamia mradi wa Kujenga Uwezo kwa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini unaojulikana kwa jina la NICHE.

Meneja wa mradi huo, Ute Jansen ameyasema hayo alipotembelea Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa Mzumbe, unatoa ufadhili kwa Shule ya Biashara na kuboresha mafunzo ya utawala wa Serikali za Mitaa.

Jansen amesema ana matumaini makubwa kuwa mradi huo utakapokamilika, utaboresha sekta
zilizoainishwa kwenye mradi huo ambazo ni kujenga uwezo katika kutoa elimu kuhusu afya, sekta binafsi na Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo nchini kupitia Shirika la NUFFIC, Johanna Van Nieuwenhuizen, amesema Uholanzi imeridhishwa na jinsi Tanzania inavyoitumia misaada kutoka nchini mwake, hivyo kujihakikishia fursa zaidi za kusaidiwa katika miradi mbalimbali.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Mugishi Nkwabi Mgasa, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, ameishukuru Serikali ya Uholanzi kwa kufadhili mradi huo na kueleza kuwa ufadhili huo una maana kubwa kwa chuo hicho kwa sababu utapanua uwezo wa chuo hicho katika kutoa mafunzo ya biashara na utawala wa Serikali za Mitaa

Thursday, September 22, 2011

PAMBAZUKO FM RADIO 90.7 MHz IFAKARA YAZIDI KUONGEZA USIKIVU.

PAMBAZUKO FM RADIO 90.7 MHz YAZIDI KUONGEZA USIKIVU

Kituo cha radio mjini Ifakara Mkoani Morogoro Panbazuko Fm sterio 90.7MHz, kwa sasa wameongeza usikivu wao kwa lengo la kuwafikia wananchi walio wengi katika sehemu mbali mbali.

Wakizungumza na mtandao huu kwa nyakati tofauti,mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho bi THERESIA MAKUNGU amesema kwa sasa wameweza kuwa na usikivu mzuri na kuwafikia wananchi walio wengi mara baada ya kumaliza kufunga mitambo yao mipya.

Bi Makungu amesema lengo kubwa la kituo chao ni kuwahabarisha wananchi yale yanayokuwa yakiendelea katika maeneo yao na duniani kwa ujumla.

Mafundi wakiimarisha mitambo ya radio pambazuko fm ifakara(picha juu)

Nae mwariri mkuu wa kituo hicho bwana ELIAS MAGANGA amesema kwa sasa wamekuwa katika wigo mpana katika kuwahabarisha wananchi wa maeneo mbali mbali ambako radio hiyo imekuwa ikirusha matangazo yake.

Maganga amesisitiza kuwa lengo kubwa la kutoa habari ni kuwajulisha wananchi yale yanayokuwa akiiendelea katika sehemu mbali mbali katika maeneo yao,na kuongeza kuwa siku zote chombo cha habari hakina ugomvi na yeyote bali vimekuwa vikitoa yale mazuri na maovu yanayofanywa katika jamii.

Wakati huo huo aliyekuwa mkuu wa wilaya ya kilombero na mkuu mpya wa mkoa wa Mwanza mheshimiwa Evarist Ndikilo ameipongeza radio pambazuko kwa juhudi zake katika kuwaelimisha na kuwahabarisha wananchi wa wilaya ya kilombero.

Ndikilo ameyasema hayo katika taarifa yake fupi aliyoitoa moja kwa moja kupitia kituo hicho cha radio katika kipindi cha JIONI LEO siku ya alhamisi alipokuwa akizungumza na wananchi wa wilaya ya kilombero katika kuwaaga kwake.

Radio Pambazuko fm kwa sasa inasikika katika mikoa ya Morogoro,Lindi ,Ruvuma na Iringa hususani katika wilaya mpya ya KILOLO

Sehemu ya antena mpya za pambazuko fm radio katika picha ya anga...

SEHEMU YA MIJI YETU INAVYOONEKANA KATIKA PICHA ZA ANGA.


Hii ni baadhi ya mitaa katika miji yetu hapa nchini Tanzania,sehemu hii inawakilisha maeneo mengi ambayo maisha ya mtanzania wa kawaida huyaendesha kila siku katika kujitafutia kipato chake cha siku..

Na hii ni kutoka katika mkoa mpya wa NJOMBE mooja ya mikoa mipya inayopatikana hapa nchini kwetu.

MKUU MPYA WA MKOA WA MWANZA AWAOMBA WAZEE KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WAPYA KILOMBERO

MKUU MPYA WA MKOA WA MWANZA AWAOMBA WAZEE KUSHIRIKIANA NA VIONGOZI WAPYA KILOMBERO
Ombi limetolewa kwa wazee kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mkuu wa wilaya atakayekuja kuongoza katika wilaya ya kilombero pamoja na viongozi wengine wanaobaki kama walivyoshirikiana vizuri na mkuu wa wilaya aliyepita.

Ombi hilo limetolewa na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya kilombero ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa mwanza mhandisi Evarist Ndikilo katika mkutano wa kuwaaga na kuwashukuru wazee wa wilaya ya kilombero uliyofanyika leo katika ukumbi wa jamosi mjini Ifakara.

Mhandisi ndikilo amewaeleza wazee, kuwa kwa kipindi cha miaka mitano aliyofanya kazi katika wilaya amefanikiwa kuleta maendeleo katika sekta ya elimu,kilimo,afya,miundombinu na mazingira,

Mbali na mafanikio hayo mhandisi ndikilo hakusita kuwaeleza wazee changamoto ambazo zinaikabili wilaya ya kilombero zikiwemo umaskini,migogoro ya Ardhi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na mifugo na kilimo cha umwagiliaji.

Kwa upande wao wazee wamezitaja changamoto zinazowakabili ikiwemo kutibiwa bure na ajali za bodaboda zinazotokea mara kwa mara ,lakini pia wamemshukuru mhandisi Ndikilo kwa ushirikiano aliouonesha kwa wazee kwa kipindi cha miaka mitano aliyokuwa akifanya kazi wilayani hapa na kumtakia kazi njema huko aendako.

SHIRIKA LA MICHE LA ITALY LATOA KOMPYUTA KWA SHULE YA MSINGI MJINI IFAKARA

SHIRIKA LA MICHE LA ITALY LATOA KOMPYUTA KWA SHULE YA MSINGI MJINI IFAKARA
Shule ya msingi ya Madukani iliyopo kata ya Ifakara wilayani Kilombero, hivi karibuni imepokea Kompyuta kumi na Printer moja kutoka shirika la MICHE la Italia.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, bibi Ester Nuruva ameueleza mtandao huu kuwa kompyuta walizopata kutoka katika shirika hilo watazitumia kwaajili ya kuwafunza wanafunzi wa kuanzia darasa la tatu hadi darasa la saba.

Aidha mwalimu mkuu huyo amesema hapo awali shule hiyo ilikuwa inafundisha somo la TEHAMA ambapo ilikuwa inahusu kompyuta kwa nadharia, kutokana na kupata msaada huo wa kompyuta sasa somo hilo litafanywa kwa vitendo.

Bibi Nuruva amesema aliyekabidhi msaada huo kwa shule hiyo alikuwa Rais wa shirika hilo, bibi Eva Maria Bardeleben kutoka Italia.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Madukani, amelishukuru shirika hilo kwakuwa na moyo wa kujitolea kwa upande wa sekta ya elimu, hivyo ameyaomba mashirika mengine kuwa na moyo wa kutoa misaada hususani katika sekta ya elimu.

AFARIKI KWA AJALI YA PIKI PIKI WILAYANI KILOMBERO-IFAKARA

AJALI YA PIKI PIKI WILAYANI KILOMBERO-IFAKARA

Mtu mmoja amekufa na wawili wamejeruhiwa kutokana na ajali ya gari iliyomgonga mwendesha pikpiki jana (20/9/011) eneo la kwa shungu kata ya Kibaoni wilayani Kilombero.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo ameieleza radio pambazuko kuwa ajali hiyo imetokea jana majira saa tisa na nusu alasiri baada ya gari hilo lenye usajili wa Na.T 184 AAC lilikuwa likiendeshwa na David Mtazama(39) mkazi wa kitongoji cha Mkuya na kumgonga mwendesha pikipiki Emanuel Amnungi(17) mkazi wa Mlabani aliyekuwa akiendesha pikipiki yenye usajili ya Na. T590 DRM ainaya TIBETA.

Aidha Chialo amemtaja aliyekufa katika ajali hiiyo ni Abdulazaki Mgoima(4) aliyekuwa amebebwa na mama yake Anna Sabu ambaye amejeruhiwa wakati wamebebwa katika pikipiki hiyo wakitokea mjini Ifakara kuelekea nyumbani kwao Kijiji cha Mbasa

Kamanda huyo amesema gari lililogonga pikipiki lilikuwa likitokea mjini Ifakara kuelekea Kibaoni na imegonga pikipiki kwa nyuma.

Amewataja majeruhi waliiojeruhiwa katika ajali hiyo ni Anna Sabu abiria wa pikipiki na dreva wa pikipiki Emanuel Mnungi ambao wote wamelazwa katika hospitali ya mtakatifu Francis ya mjini Ifakara katika wodi ya wagonjwa mahututi.

Hata hivyo kamanda Chialo amesema dreva amejisalimisha polisi na tayari leo amekwisha fikishwa mahakamani kujibu mashitaka manne ya kusababisha kifo, kusababisha majeruhi wawili na uharibifu wa mali.

MBUNGE WA MIKUMI ACHANGIA SHILINGI MILIONI 27.3KWA MIRADI YA MAENDELEO

MBUNGE WA MIKUMI ACHANGIA SHILINGI MILIONI

Mbunge wa jimbo la Mikumi kwa tiketi ya CCM, bwana Abdulsalam Ameri hadi sasa kwa muda wa miezi kumi akiwa mbunge, amekwisha tumia jumla ya shilingi milioni 27.3 kwa kuchangia miradi ya maendeleo ya kata.

Bwana Ameri amesema jimbo lake la mikumi lina jumla ya kata 14 na yuko katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagu kuwa mbunge na kupita kata hadi kata.

Amesema hadi Septemba 20 mwaka huu amekwisha tembelea kata kumi kwa kufanya mikutano ya kuwashukuru na kupata kero kutoka kwa wananchi wa kata husika.

Hivyo amewataka wananchi wa jimbo hilo kuwa uchaguzi umekwisha mwaka 2010 na makundi yamekwisha sasa imebaki kufanyakazi ya kujenga uchumi wa nchi yetu na amewataka viongozi wa serikali za kata wafanye kazi isiyokuwa na jazba.

Aidha mbunge huyo amewaasa viongozi waache kufuata makundi, wafanye kazi waliyotumwa pia amewataka viongozi wa vijiji kuwasomea taarifa ya mapato na matumizi wananchi wa vijiiji vyao kwa kila kipindi cha miezi mitatu ili wananchi wawe na imani na viongozi wao na kuhamasika kujiletea maendeleo.

WANANCHI WA KIDODI WILAYANI KILOSA WACHANGA SHILINGI MILION TATU KWA AJILI YA MRADI WA MAJI.

SHILINGI MILION TATU KWA AJILI YA MRADI WA MAJI.

Jumla ya shilingi mil.3 zimekusanywa kutokana na mchango wa wananchi wa kijiji cha lumango kata ya kidodi wilayani kilosa kwaajili ya mradi wa maji ya mtiririko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na afisa mtendaji wa kijiji hicho sept 18 mwaka huu katika mkutano wa hadhara uliofanyika katia kata ya kidodi kwa mbunge wa jimbo la mikumi bwana Abdulsalam Amer,imeeleza kuwa kijiji hicho kimepangiwa kuchangia mradi huo kiasi cha shilingi mil 4 na laki 5.

Taarifa hiyo iliyowasilishwa kwa mbunge wa jimbo hilo imeeleza kuwa wananchi wa kijiji hicho hadi sasa wanadaiwa shilingi mil 1 na laki 5 kwa ajili ya mradi hou.

Diwani wa kata ya kidodi bwana Ibrahim Fatahaki amesema kuwa katika kata hiyo,kijiji cha lumando kinaongoza kwa mchango wa mradi wa maji katika kata ya kidodi.

Wakati huohuo wananchi wa kijijik hicho wamfyatua jumla ya matofali 20000 ya kuchoma kwa ajili ya ujenzi wa zahanati unaotarajia kuanza hivi karibuni.


Hata hivyo mbunge wa jimbo hilo bwana Amer ameahidi kusaidia ujenzi wa zahanati hiyo kwa kutoa vifaa vya ujenzi.