BOMBA LA MAFUTA LAPASUKA WILAYANI KILOSA
Jumla ya ekari 1400 za mazao mbalimbali katika kata ya Malolo wilayani Kilosa Mkoani Morogoro,zimeharibiwa na mafuta machafu yanayovuja kutoka katika bomba kubwa linalosafirisha mafuta hayo kutoka Tanzania kwenda Zambia lililopita katika kata hiyo.
Afisa kilimo cha umwagiliaji wa kata hiyo, Bwana Mwelasi amesema bomba hilo la mafuta tangu lipasuke hadi sasa ni muda wa miezi miwili na limeharibu mfumo wa umwagiliaji wa mashamba jumla ya ekari 500 ya mazao ya vitunguu na mahindi.
Bwana Mwelasi ameyataja mazao yaliyoathirika kutokana na kupasuka kwa bomba hilo kuwa ni vitunguu na mahindi ambapo hata kiwango cha uzalishaji wa mazao hayo amesema kuwa kimeshuka.
Afisa kilimo huyo amesema mimea imekauka kutokana na mafuta yanayovuja kutoka katika bomba hilo na kuingia chini ya ardhi na kuathiri mazao na kusababisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji.
Akizungumzia uzalishaji wa mazao katika kata hiyo Amesema hapo awali kabla ya bomba hilo kupasuka ekari moja ilikuwa ikizalisha magunia 70 ya mazao, lakini sasa ekari moja inazalisha gunia 20 ya mazao kiwango ambacho amesema kimeshuka kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo amevitaja Vijiji vilivyoathirika na mafuta hayo kuwa ni Malolo "A", Malolo "B" na Mgogozi ambapo wananchi wanaoishi katika vijiji hivyo wamo hatarini kuharibu afya zao kutokana na maji wanayotumia kwa kunywa na shughuli zinigine.
Kutokana na athari hiyo kutokea Mbunge wa jimbo la Mikumi, bwana Abdulsalam Ameri tayari amekwisha peleka mtambo wake wa kuchimba visima vya maji katika kata hiyo na kila kijiji kati ya vijiji hivyo vitachimbiwa visima viwili na kufanya idadi ya visima sita katika kata hiyo ambavyo vitasaidia kuokoa maisha ya wananchi wa kata hiyo.
No comments:
Post a Comment