Friday, September 23, 2011

TANZANIA KUNUFAIKA NA MSAADA WA EURO MILIONI 15 KUTOKA SERIKALI YA UHOLANZI

TANZANIA KUNUFAIKA NA MSAADA WA EURO MILIONI 15

TANZANIA itafaidika na msaada wa Euro milioni 15 ambazo ni sawa na (zaidi ya Sh bilioni 30 za kitanzania ) kutoka Serikali ya Uholanzi kugharamia mradi wa Kujenga Uwezo kwa Vyuo vya Elimu ya Juu nchini unaojulikana kwa jina la NICHE.

Meneja wa mradi huo, Ute Jansen ameyasema hayo alipotembelea Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro, kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ambao kwa Mzumbe, unatoa ufadhili kwa Shule ya Biashara na kuboresha mafunzo ya utawala wa Serikali za Mitaa.

Jansen amesema ana matumaini makubwa kuwa mradi huo utakapokamilika, utaboresha sekta
zilizoainishwa kwenye mradi huo ambazo ni kujenga uwezo katika kutoa elimu kuhusu afya, sekta binafsi na Serikali za Mitaa.

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo nchini kupitia Shirika la NUFFIC, Johanna Van Nieuwenhuizen, amesema Uholanzi imeridhishwa na jinsi Tanzania inavyoitumia misaada kutoka nchini mwake, hivyo kujihakikishia fursa zaidi za kusaidiwa katika miradi mbalimbali.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Mugishi Nkwabi Mgasa, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, ameishukuru Serikali ya Uholanzi kwa kufadhili mradi huo na kueleza kuwa ufadhili huo una maana kubwa kwa chuo hicho kwa sababu utapanua uwezo wa chuo hicho katika kutoa mafunzo ya biashara na utawala wa Serikali za Mitaa

No comments:

Post a Comment