Thursday, July 27, 2017

VIONGOZI WAASWA KUSIMAMIA SERA YA ELIMU BURE ILI KUKUZA KIWANGO CHA ELIMU

Maafisa elimu kata na wenyeviti wa shule zote Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wametakiwa kuelimisha jamii juu ya tamko la Serikali la elimu bure ili wawe makini kufuatilia mienendo ya watoto pindi wawapo shuleni kwa kujenga taratibu za kuwachunguza iwapo wanafuatilia masomo yao au lah.

Wito huo umetolewa Julai 27 mwaka huu na afisa elimu Taaluma Mohamed Mwingilihela wakati wa mafunzo ya siku 3 yanayoendelea katika ukumbi wa Shule ya msingi Mazinyungu yaliyoanza Julai 25 mpaka Julai 28 kwa lengo la kutoa elimu kwa maafisa elimu kata na na viongizi mbalimbali wa shule jinsi ya kuwaelimisha wananchi wanaowazunguuka kujenga utaratibu wakuwafuatilia watoto wao pindi wawapo masomoni.

Mwingilihela amesema wanajamii wamesahau majukumu yao kwa kufuatilia masomo na mienendo ya watoto kwa kuwaacha wakizurula badala ya kukaa na kujisomea nakwenda kwenye mabanda ya video yaliyopo kila kona kwenye vijiji ambayo watumiaji wakubwa wa mabanda hayo ni wanafunzi hao.

Sambamba na hayo amewataka wazazi kuchangia michango midogo ya shule inayowahusu ikiwemo michango ya chakula cha mchana cha wanafunzi na michango mingine   ikiwemo ya miundombinu ya barabara kwani michango hiyo ipo nje na tamko ka serikali la elimu bure.

Aidha nae Mtendaji elimu kata kutoka Ulaya Wilayani Kilosa Rehema Kakwembe amesema wameyapokea kwa mtazamo chanya mafunzo hayo na watahakikisha kufikisha elimu tosha kwa jamii zote Wilayani hapa juu ya kushiriki katika michango inayowahusu hasa kufanikisha wanafunzi katika shule zote wanapata chakula cha mchana mashuleni vilevile kuwazuia watoto wao kwenda kwenye mabanda ya video na badala yake kuutumia muda huo katika kujisomea.

No comments:

Post a Comment