TAARIFA YA HALI YA UKIMWI KATIKA WILAYA YA NJOMBE SIKU YA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI DISEMBA MOSI 2010 KATIKA KIJIJI CHA KICHIWA KATA YA IGONGOLO.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Leo ni mara ya Tano tangu mwaka 2006 kwa kufanya maadhimisho rasmi ya Kitaifa ya Siku ya UKIMWI Duniani katika Wilaya ya Njombe.
Mwaka huu 2010 Kitaifa maadhimisho ya Siku hii yatafanyika katika Manispaa ya Morogoro uwanja wa Nane Nane.
Ujumbe wa Mwaka 2010 ni “MWANGA KWA HAKI”
…..Wadau Wote wanatakiwa kutoa na kutetea upatikanaji wa huduma na haki za binadamu kwa watu Wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI….
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kimsingi wakati tunatafakari ujumbe huu katika maadhimisho haya nia kubwa ni kuihamasisha jamii iweze kutambua kuwa hali ya UKIMWI Wilayani Njombe ina athari kubwa na kuwa janga la UKIMWI linaathiri mtu binafsi,familia,jamii,Wilaya,Mkoa na Kitaifa.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Ifahamike wazi kuwa madhara yanayotokana na maambukizi ya UKIMWI ni makubwa kwa kila mwananchi,jitihada kubwa zinafanyika kitaifa na Kiwilaya za kukabiliana na UKIMWI kwa kutoa elimu na huduma za kuzuia maambukizi mapya,tiba na huduma kwa watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI hata hivyo bado changamoto ni nyingi sana katika Wilaya yetu.
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni:
i.Ongezeko la huduma za utoaji dawa za tiba endelevu katika Vituo vya Vijijini mfano Kidugala,Lupembe na Makambako ili kusogeza huduma karibu na Wananchi
ii.Kuendelea kupokea fedha toka Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania ambapo kwa Mwaka 2009/10 Wilaya imepokea jumla ya Tsh.114,974,000 kati ya fedha hizo Tsh.77,259,000 zimepokelewa na Halamshauri ya Wilaya ya Njombe na Sh.37,715,000 zimepokelewa na Halamsahuri ya Mji wa Njombe kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya Kudihibiti UKIMWI ikiwemo ya kuhudumia watoto Yatima,Watu Wanaoishi na VVU pia kutoa elimu ya mapambano dhidi ya UKIMWI kwa makundi mbambali.
iii.Wilaya imeendelea kupata misaada na huduma kutoka kwa Wadau kama TUNAJALI,JPIEGO,fhi-ROADS Project,Asasi za Kidini na Kiraia na Wanachi kwa ajili ya mapambano dhidi ya UKIMWI
HALI YA MAAMBUKIZI YA UKIMWIMheshimiwa Mgeni Rasmi,
Katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2010 jumla ya Watu 13,481 walijitokeza kupima VVU kati yao Wanaume 4,561 na Wanawake 8,920 ambapo waliogundulika kuwa na VVU ni 3,436 kati yao Wanaume 1,407 na Wanawake 2,029 Sawa na asilimia 25.4 hii ni kutokana na idadi ndogo ya Watu waliojitokeza kupima katika kipindi husika.
Watu walipima kwa hiari(VCT) ni 4,235 kati yao wanawake 3047 na Wanaume 1,188 walipima VVU na Wanawake 8,920.
Wanawake wajawazito 4,918 na Wenza 2,671 walipima VVU kati yao Wajawazito 557 na Wenza 338 waligundulika kuwa na VVU
Huduma ya kuzuia maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto ni mojawapo ya njia inayotumika hapa wilayani. Huduma hii ni njia ya uhakika zaidi ya kujua hali ya maambukizi ya UKIMWI katika jamii na pia husaidia kuzuia maambukizi kwa watoto wanaozaliwa na wazazi wenye virusi vya UKIMWI kwani hupatiwa dawa husika.
Pia Jumla ya Watu 1,657 kati yao Wanaume 702 na Wanawake 955 walipatiwa huduma ya maalum ya Unasihi na upimaji VV (PITC) ambapo wenye VVU ni 605 kati yao Wanaume ni 245 na Wanawake ni 360
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Viashiria vya kiwango cha kuenea kwa kasi kwa UKIMWI vinaoneshwa pia na hali ya maambukizi ya magonjwa ya ngono.
Katika wilaya ya Njombe hali ya maambukizi ya Magonjwa ya ngono imekuwa ikiongezeka kwa kasi kubwa toka wananchi 2,247 waliotibiwa mwaka 1994 hadi wananchi 15,208 kwa mwaka 2006.
Kwa kipindi cha Januari –Septemba, 2010 Jumla ya Watu 2,507 walitibiwa magonjwa ya ngono kati yao Wanaume ni 957 na Wanawake ni 1550
Idadi kubwa ya watu wanaojitokeza kutibiwa Magonjwa mbalimbali yakiwemo ya Ngono inatokana na wananchi kuzingatia elimu inayotolewa kwa jamii. Hata hivyo hali hii inadhihirisha kuwa watu wengi bado hawajabadili tabia ya kufanya ngono isiyo salama, hii inatokana aidha na uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya kondomu, upuuziaji, kutopatikana au kutokuwa na uwezo wa kununua kondomu au makusudi ya kutotumia kondomu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Hali ya maambukizi ya Ukimwi ni kubwa katika Kata za Njombe Mjini, Makambako, Imalinyi, Ilembula, Mtwango, Mdandu, Lupembe na Kidegembye. Hali hii inadhihirishwa na kuwepo kwa wagonjwa wengii wa muda mref, watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI,Idadi kubwa ya watu wanaogundulikwa kuwa na Virusi vya UKIMWI na ongezeko kubwa la Watoto Yatima
Mheshimiwa Mgeni rasmi,
Sababu za Kata husika kuwa na maambukizi makubwa ya virusi vya UKIMWI ni;
Muingiliano wa Wageni wanaofuata huduma mbalimbali kama hospitali ya Ilembula, Biashara ya mbao, viazi, makampuni/mashamba ya chai katika miji na Vijiji vya Makambako,Ilembula,Lupembe nakadhalika.
Shughuli za kibiashara na ajira za kuhamahama kama mashamba ya chai, upasuaji mbao na viazi.
Baadhi ya Waganga wa Jadi wanawadanganya wananchi kuwa wanaouwezo wa tiba ya UKIMWI.
Imani za kishirikina za korogwa na baadhi ya wagonjwa wanaorudishwa nyumbani kutoka Miji mingine.
Kukosekana kwa uelewa sahihi wa UKIMWI miongoni mwa Jamii (Kuhudumia wagonjwa, kutobadili tabia juu ya ngono salama.
Mila na desturi ya Kutotahiri wanaume.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Huduma kwa Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI :
Kwa mwaka 2009/2010 Halmashuri ya Wilaya ya Njombe imewezesha fedha Tsh.Milioni Tano kwa ajili ya mitaji ya miradi ya kiuchumi kwa Vikundi 10 vya WAVIU yaani Tumaini-Kidugala,Amani–Itunduma,Upendo-Ukalawa,PIUTA-Ulembwe,Twendepamoja-Ihang’ana,SemaUmasikiniBasi(SEUBA)-Makambako,Ngalinjele-Luduga,Tunajua-Iyayi na MaishaBora-Wangama.
ATHARI ZA UKIMWI WILAYANI NJOMBE
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Kutokana na athari za UKIMWI,
Wilaya ya Njombe inakabiliwa na ongezeko kubwa la Watoto Yatima wanaokadiriwa kufikia 12,000 katika Wilaya.
Jitihada za Wilaya kwa kushirikiana na wadau hususani Mradi wa Tunajali
(FHI) imefanya Utambuzi unaoshirikisha jamii wa Watoto wanaoishi katika Mazingira Hatarishi zaidi(WWMHZ) ambao umefanyika katika Wilaya kati ya Mwaka 2007-2010 umefanikisha kuwatambua Watoto Yatima na Wanaoishi katika Mazingira Hatarishi zaidi ni kama ifuatavyo:
Mwaka H/W ya Njombe H/ Mji wa Njombe Jumla Kiwilaya
2009/10 Wav Was Jml Wav Was Jml Wav Was Jumla
2,521 2,341 4,862 1,920 2,116 4,036 4,441 4,457 8,898
Hadi sasa utambuzi wa Watoto Yatima na Wanaoishi katika Mazingira hatarishi Zaidi umefanyika katika Kata 13 za Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya ni Kata 10 tu kati ya Kata 36 umefanyika bado Kata 26 katika H/Wilaya ya Njombe ambapo Jitihada kwa kuwasilisha maombi ya fedha zinaendelea na kushirikisha Wadau wa ndani na nje yaani Mashirika yasiyo ya Kiserikali,Wizara za Afya na Ustawi wa Jamii na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia na Watoto ili kufanikisha utambuzi wa Watoto wote Wanaoishi katika Mazingira hatarishi wilayani Njombe.
Watoto yatima waliopata huduma Mwaka 2009/10 ni kama ifuatavyo:
Kwa mwaka 2009/10 Halmashauri ya Wilaya imetoa fedha Jumla ya Tshs. 16,200,000/= kwa ajili ya Watoto Yatima 324 kwa ajili ya mahitaji ya elimu katika Shule za Sekondari na Jumla ya Watoto 262(Wav. 132 na Wasichana 130) Wanaolelewa katika Vituo vya Ilembula ELCT,Kipengere RC,Kituo cha Tumaini-Ilunda ,Upendo Nyombo na Jumuiya ya Orphans Education Centre –Makambako wamepatiwa Jumla ya Shs.5.000,000/=(Milioni Tano)kwa ajili mahitaji ya kielimu na tiba kutokana na fedha toka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania.
Pia Halmashauri ya Wilaya imeandaa gunia 5 za Mchele ,katoni 20 na mafuta ya kupikia ndoo 5 vyenye thamani ya Jumla Sh.1,025,000/=kwa Vituo vya Kulelea Watoto Yatima husika ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii kutoa misaada kwa Watoto yatima wakiwemo wanaolelewa katika Vituo vya Watoto yatima.
Kadhalika kwa Mwaka 2009/10 Mashirika ya NDO-RC (Njombe Development Organisation) imetoa misaada ya vifaa vya elimu,afya na mahitaji muhimu kwa Watoto Yatima Jumla 6,074 yenye thamani ya Sh.228,054,750 na Shirika la TUNAJALI(FHI) limetoa msaada wa Jumla ya Watoto Yatima 2,463 na Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wamepatiwa misaada ya thamani Jumla Tsh.121,509,000
Pia Mradi wa ROADS –Makambako umetoa msaada kwa Watoto Yatima 1,738 kati yao Wavulana 798 kwa fedha Tsh 49,678,600/= na Wasichana 830 kwa kuwahudumia fedha za mahitaji ya shule,chakula,tiba, malazi na msaada wa kiasaikolojia na WAVIU 1,320 kati yao Wanaume 480 na Wanawake 840 kwa ajili ya huduma za chakula,matibabu na vifaa vya nyumbani vya thamani ya Sh 37,993,140/=
Jamii inapaswa kuhakikisha inawasaidia Watoto yatima na kuwahudumia Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI na kwa kuanzisha mifuko maalum kila Kijiji mfano wa Mtaa wa Ubena Kata ya Ubena-Makambako kimeanzisha mfuko wa Yatima ambapo wananchi wamechangia Sh.Milioni Moja nab ado michango inaendelea hivyo kila Kijiji kinapaswa kuiga mfano huo.
Athari nyingine ni:
Kupungua kwa nguvu kazi na kupungua uwezo wa kiuchumi wa familia kutokana na wanafamilia kuuguza wagonjwa kwa muda mrefu.
Gharama kubwa kwa Serikali na jamii katika kuhudumia Watoto Yatima na Watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI
Mifarakano katika Familia na jamii kutokana na unyanyapaa.
CHANGAMOTO KATIKA KUPAMBANA NA JANGA LA UKIMWI.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Serikali na Halmashauri kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali inafanya jitihada kubwa sana katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI hata hivyo tanakabiliwa na changamoto zifuatazo:-
Uchache wa vituo vya ushauri nasaha na upimaji wa VVU hususani maeneo ya Vijijini.
Uchache wa vituo vya huduma na kutoa tiba kwa Wagonjwa na Wato wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kutokana na ongezeko na muingiliano wa watu na ukubwa wa Wilaya.
Upungufu wa vifaa,dawa na vitendanishi (reagents) kwa ajili ya upimaji wa VVU
Upungufu wa watumishi hususani wa maabara katika vituo vya afya ambao wangesaidia upimaji wa VVU.
Ongezeko la wagonjwa wa UKIMWI kutokana na kushamiri kwa biashara mbalimbali katika Wilaya yetu sambamba na kuendelea kwa Mila na desturi potofu za ukeketaji wasichana, kutotahiri wavulana na wasichana wanaotarajia kuolewa kufanya ngono na watu wazima kwa nia ya kufungua njia ya uzazi.
MIKAKATI YA KUPAMBANA NA UKIMWI
Mheshimiwa Mgeni Rasmi,
Halmashauri ina mikakati ifuatayo katika kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI:-
Kuongeza vituo vya ushauri nasaha,tiba endelevu na upimaji VVU hususani Vijijini ili kusogeza huduma hii muhimu karibu zaidi na Wananchi.
Kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo Wilayani zikiwemo asasi zisizo za kiserikali kwa mfano AMREF, FHI-PROGRAMU YA TUNAJALI , SHIPO, GROWOYODA, Benjamin Mkapa Foundation,ENGENDER HEALTH, (JohnHopkins University)JPIEGO,SPW, PSI, CUAMM, NJODINGO , PADA, TY-SEDA nk. katika juhudi za kupambana na UKIMWI.
Kuendelea na juhudi za Kuhamasisha akinamama wajawazito na Wenzi wilayani kuhusu umuhimu wa kuanza kliniki mapema na kupimwa Virusi vya UKIMWI kama wana maambukizi ili wapatiwe dawa ya kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.
Kuendelea kutoa dawa za kupunguza makali ya VVU.
Kuhamasisha jamii katika Kata zote ili kuchukua jukumu la kutunza watoto yatima na watoto waishio katika mazingira magumu na hatarishi.
Kuendelea kuelimisha jamii njia ya kupambana na ugonjwa wa UKIMWI kwa kuimarisha kamati za Ukimwi za Wilaya, kata, vijiji na vitongoji vyake.
Kusimamia na kuendeleza mpango wa wilaya wa mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI.
Kushirikiana na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS katika juhudi za kupambana na UKIMWI.
Kuhamasisha jamii kuacha mila za ukeketaji sambamba na kuhimiza wavulana/Waname kutahiri na watu wote kujitokeza kupima afya kwa hiari na kukomesha unyanyapaa katika Jamii