HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA NJOMBE MH.SARA DUMBA KATIKA SIKU YA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI 1 DISEMBA 2010.
Waheshimiwa Viongozi wa Wilaya, Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara, Maafisa Tarafa, Maafisa Watendaji wa kata, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Wazee wetu na Ndugu wananchi wa Tarafa ya Makambako,
KAMWENE,
BWANA YESU ASIFIWE
TUMSIFU YESU KRISTU,
SALAAM ALEIKUM!!!
Ndugu Wananchi,
Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii ya pekee kuwashukuru viongozi wote Tarafa ya Makambako , Kata ya Igongolo, Kijiji cha Kichiwa kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika siku hii muhimu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani na kunipa nafasi ya pekee ya kuwa mgeni rasmi.
Siku ya leo ya Tarehe 1 Disemba 2010 tumekusanyika hapa kwa lengo la kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani inayoadhimishwa Duniani kote katika kuhamasisha jamii katika mapambano dhidi ya UKIMWI na kutafakari madhara yanayotokana na janga hili la UKIMWI, vile vile kuikumbusha jamii kuweka mikakati ya kupambana na UKIMWI kwa dhati. Ujumbe wa mwaka huu ni “MWANGA KWA HAKI” Wadau wote kutoa na kutetea upatikanaji wa huduma na haki za binadamu kwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Ndugu Wananchi,
Tangu UKIMWI ulipogundulika Nchini mwaka 1983 Serikali imeweka mipango mbalimbali ya Mapambano dhidi ya UKIMWI ikiwa ni pamoja na kuadhimisha Siku hii ya tarehe Mosi Disemba inayoendana na upimaji wa hiari wa virusi vya ukimwi.
Ndugu wananchi,
Njombe kama zilivyo wilaya nyingi nchini ni miongoni mwa Wilaya zinazokabiliwa na ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya Ukimwi miongoni mwa Wananchi.
Ndugu wananchi,
Unyanyapaa unasababisha maambukizi yazidi kuongezeka kwa kuwa watu wanaficha hali zao na kufanya ngono zisizo salama na wengine kutojitokeza kupima.
Ndugu wananchi,
Ni ukweli usiopingika kuwa Elimu juu ya Ukweli kuhusu UKIMWI imetolewa nchini na kwa wilaya yetu kwa kiwango kikubwa lakini bado idadi ya watu wanaojitokeza kupima ni ndogo sana na kwa wakati huohuo hali ya maambukizi imefikia Asilimia 25.4% kwa waliopimwa katika Vituo vya Ushauri Nasaha kuanzia Januari hadi Septemba, 2010.
UPIMAJI WA HIARI WA VIRUSI VYA UKIMWI
Ndugu wananchi,
Tangu Ukimwi ulipogundulika nchini Tanzania mwaka 1983 maambukizi ya UKIMWI yameendelea kuongezeka na kusambaa kwenye Mikoa na Wilaya zote.
Katika Wilaya yetu ya Njombe, wagonjwa wa kwanza Watatu(3) waligundulika katika Hospitali ya Ilembula mwaka 1986 ambako upimaji wa Virusi vya UKIMWI ulianza kufanyika. Na hali ya maambukizi mapya imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Watu waliojitokeza kupima tangu Julai 2005 hadi Septemba 2010 ni 80,415 kati yao 41,204 ni Wanaume na 59,577 ni Wanawake. Waliogunduliwa kuwa na Virusi vya UKIMWI ni 17,093 ambapo kati yao Wanaume ni 6,538 na Wanawake ni 10,555 Hivyo kiwango cha maambukizi ya UKIMWI kufuatia upimaji huu ni 19.2%.kama jedwali Na. 1 hapa chini linavyoonyesha takwimu ya Upimaji kwa ufupi tangu mwaka 2005/06 hadi Septemba 2010
Jedwali na 1: Upimaji wa virusi vya UKIMWI
Idadi ya waliopima Wenye Virusi
Me Ke Jumla Me Ke Jumla
2005/06 2,725 2,262 4,987 372 540 912 18.2%
2006/07 4,029 4,315 8,345 600 890 1,490 17.9%
2007/08 23,779 37,323 61,102 3,089 5,491 8,580 14.0%
2008/09 6,110 6,757 12,867 1,070 1,605 2,675 20.7%
Jan – Sept
2010 4,561 8,920 13,481 1,407 2,029 3,436 25.4%
JUMLA 41,204 59,577 80,415 6,538 10,555 17,093 19.2%
Chanzo: Idara ya Maendeleo ya Jamii
Ndugu wananchi,
Hali ni mbaya zaidi kwa kuwa inaonyesha watu wengi wanazidi kupata maambukizi ya magonjwa ya ngono kwani kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2010 hadi Septemba, 2010 kati ya wagonjwa waliofika hospitali ya Wilaya ya Njombe kutibiwa magonjwa mbalimbali , jumla ya watu ..... waligundulika kuwa na magonjwa ya ngono wakiwemo wanaume .... na wanawake .... , idadi hii ni kubwa kwani magonjwa ya ngono ni moja ya viashiria vya ukubwa wa maambukizi ya UKIMWI kwani tafiti nyingi zinadhihirisha kuwa asilimia ........ya watu wanaougua magonjwa ya ngono huwa na maambukizi ya UKIMWI.
Ndugu Wananchi,
Suala la hofu ya kupima na kubainika kuwa na maambukizi inabidi mlipinge vikali kwani baada ya mtu kugundulika ameambukizwa Ukimwi ataweza kupata huduma za dawa ya kupunguza makali ya Ukimwi katika sehemu mbalimbali mfano Hospitali ya Njombe TANWAT na Ilembula na kupata ushauri nasaha na hivyo kumuwezesha kuendelea na maisha yake kama kawaida.Mtu ukipima na kujua hali yako utajua ni namna gani uishi na hivyo utajiongezea muda mrefu wa kuishi.
Kadhalika Wilaya imeweka mpango wa kuanzisha vituo vingine vya kutoa dawa za kupunguza makali ya Ukimwi katika Zahanati ya Kipengere,Kituo cha Afya cha Makambako na Lupembe ili kuwapunguzia gharama za Usafiri wa kufuata huduma hizo Wilayani.
Ndugu Wananchi,
Napenda kuwashukuru sana wale wote waliojitokeza kupima UKIMWI kwa hiari, na kwa wale ambao hawakujitokeza basi nawaomba waende wakapime ili kwa pamoja tuweze kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI wilayani Njombe.
Pia sote tutambue kuwa tunawajibu wa kuwasaidia Watoto yatima na Waathirika wa ukimwi.
No comments:
Post a Comment