Thursday, July 3, 2014

MBUNGE WA JIMBO LA MIKUMI AWATOA WASIWASI WAKAZI WA MIKUMI JUU YA MRADI WA MAJI MIKUMI WILAYANI KILOSA MKOANI MOROGORO


Imeelezwa kuwa licha ya Mwenge wa Uhuru kupita katika Tarafa ya Mikumi Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji ambapo mpaka sasa hayajaanza kutoka katika Tarafa hiyo.
                                                        mradi wa maji mikumi

Hayo yameelezwa na baadhi ya wananchi wa Tarafa ya Mikumi Shafii Makiwa na Gaudensia Aloyce wakati wakizungumza na HABARIKWANZA julai mbili mwaka huu.
Wananchi hao wamesema kuwa tatizo la ukosefu wa maji katika Tarafa hiyo ni la muda mrefu kwani tangu Mwenge wa Uhuru kuzindua mradi wa maji safi na salama hadi sasa hakuna jitihada zinazofanyika ili kuhakikisha changamoto ya maji inatatulika katika Tarafa hiyo hali inayosababisha maisha kuzidi kuwa magumu siku hadi siku.
Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Mikumi Abdusalama Amer maarufu kwa jina la Sasgas wakati akizungumza na HABARIKWANZA amekiri kutokuwepo kwa maji katika Tarafa hiyo na kuahidi maji yataanza kutoka mapema mwezi wa nane mwaka huu.
                              Mbunge wa jimbo la mikumi Abdulsalama Amer
Amer amesema kuwa sababu ya kutokutoka kwa maji kwenye mradi huo ni kutokana na mkandarasi kuishiwa fedha za kumalizia mradi wa maji kwa wakati lakini kwa sasa fedha imepatikana kwani bajeti hiyo imeshapitishwa Bungeni Mjini Dodoma hivi karibuni.

Aidha Mbunge huyo amewatoa wasiwasi wananchi wa Tarafa ya Mikumi kwa kusema kuwa maji safi na salama lazima yatoke katika maeneo hayo kwani atahakikisha anatatua changamoto zote zinazowakabili hususani ya maji safi na salama. 

MKUU WA WILAYA YA KILOSA ELIAS TARIMO AMEWATAKA WAHUDUMU WA AFYA WILAYANI KILOSA KUFUATA KANUNI NA TARATIBU ZA KAZI WAWAPO KAZINI



Mkuu wa wilaya kilosa mkoani morogoro Elias Tarimo amewataka wahudumu wa sekta ya afya wilayani humo kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata maadili ya kazi zao.
Ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa kikao na wajumbe wa baraza la wazee wilaya, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri wilaya,Viongozi wa vyama vya siasa na Baadhi ya wataaramu wa aiadaza za Halmashauri ya wilaya kilosa.
Tarimo ameyasema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na wazee wa baraza hilo,ya kuwa wahudumu wa afya katika hospitali ya wilaya ,wanatabia ya kuwatolea lugha chafu mara wanapofika kwa ajili ya kupata matibabu hospitalini hapo.
Aidha amesema kuwa wanapaswa kuhudumia wagonjwa kwa kauli nzuri na upendo kwa wagonjwa wanahitaji kupokea na kupatiwa huduma kwa faraja si kuwatolea lugha chafu,ambapo baadhi wamekuwa wakitoa malalamiko kila siku juu ya watoa huduma hao wa sekta ya afya huwafokea na kuwanyanyasa wagonjwa.
Ameongeza kwa kusema kuwa changamoto zinazovikabili vituo vya afya wilayani humo zikiwemo dawa na watoa huduma,amesma serikali itaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo ikiwemo kutoa kipaumbele kwa wazee kwa kuandaliwa kadi za matibabu ili wazitumie mara wanapokwenda kupata matibabu.

MTOTO MWENYE UMRI WA MIAKA MITATU ATELEKEZWA NA MAMA YAKE MZAZI WILAYANI KILOSA MKOANI MOROGORO


Mama mmoja anayefahamika kwa jina la Mwamini Juma [20] mkazi wa mamoyo wilayani Kilosa mkoani Morogoro anadaiwa kumtelekeza motto Selemani Salumu mwenye umri wa miaka mitatu (3) kwa shangazi zake naye kwenda kwa wanaume.

Kwa majibu wa shangazi zake Mwamini Juma ambaye  ni mwasham Salumu na Halka Salum wamesema kuwa motto wao huyo mwamini salumu ambaye ni motto wa kaka yao anatabia ya kumtekeleza mtoto mara kwa mara na kwenda kwa wanaume wengine huishi nao na mwisho wa siku naye huachwa.

Aidha wamesema kuwa mtoto Mwamini Juma alipewa mimba akiwa na umri wa miaka 17 na kijana anayefahamika kwa jina la Doto salumu mkazi wa mamoyo wilayani Kilosa mkoani Morogoro ambapo mwaka 2011 alimpa mimba mtoto waliongea juu ya matunzo ya mtoto na kukubaliana katika malezi ya kumlea mtoto atakayezaliwa lakini kijana huyo hakufanya hivyo na kuamua kutoroka majukumu ya kumtunza mwanaye.

Kwa upande wake mama wa mtoto Selemani Salumu ambaye anasadikisha kumtelekeza mtoto wake mara kwa mara amethibitisha kumtelekeza mtoto wake huyo na kwenda kwa wanaume na kusema kuwa siku alipoondoka nyumbani kwa mara ya mwisho alielekea  chanzuru ambapo huko alienda kwa Ally Mkubuge akidai kuwa ni rafiki yake . Na kufafanua kuoa  anapotoroka huwa anaogopa kurudi nyumbani mapema kutokana na shangazi zake kumpiga kwa kile anachokitenda cha kutoroka na kumuacha mtoto nyumbani.

Wednesday, July 2, 2014

UJENZI WA KANISA LA AGLIKANA KATIKA KIJIJI CHA DODOMA ISANGA WAKAMILIKA



Diwani wa kata ya masanze wilayani kilosa mkoani morogoro Jonathani Kambikiye ameongoza harambee ya uchangiaji wa vifaa vya ujenzi wa kanisa la Aglikana kijiji cha Dodoma Isanga kilichopo kwenye kata hiyo.
Harabee hiyo imefanyika hivi karibuni baada ya Ibada ya jumapili ambayo imeongozwa na mchungaji Mwegalawa wa kanisa la Aglikana parishi ya zombo na Area Dean wa dinari ya zombo.
Kambikiye ameongoza zoezi hilo  la harambee ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ambapo waumini wa kanisa hilo la kijiji cha Dodoma Isanga na viongozi na wadau mbalimbali wameweza kukamilisha vifaa vyote kwa ajili ya kuezekwa kanisa hilo ambalo lilianzishwa mwaka 1983 vimeweza kukamilika hivyo kuwa na uhakika wa ujenzi huo wa nyumba ya Mungu.
Vifaa vilivyokuwa vikihitajika ni pamoja na bati 30 mbao 70 na misumari kilo 15 ambapo Diwani huyo amechangia bati tano na kilo nne za misumari ili kuwapa nguvu waumini hao kwa ajili kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo.
Akizungumza  baada ya harambee hiyo Diwani huyo wa kata ya Masanze Jonathani Kambikiye amewashukuru wote waliochangia vifaa hivyo ili kukamilisha ujenzi huo wa kanisa na kuwataka wazee wa kanisa hilo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo zoezi hilo la nyumba ya Ibada.

WAKAZI WA WILAYANI KILOSA MKOANI MOROGORO WATAKIWA KUJIANDAA NA ZOEZI LA USAJILI NA UTAMBUZI KWENYE DAFTARI LA WAKAZI



Wakazi wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wametakiwa kujiandaa na zoezi la usajili na utambuzi kwenye daftari la wakazi katika maeneo yao wanayoishi ili kupata kitambulisho cha Taifa ambacho ni muhimu kwa kila Mtanzania aliyefikisha umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Elias Tarimo ofisini kwake wakati akizungumza kwenye kikao maalum kilichowahusisha Wakuu wote wa Idara na Viongozi mbalimbali Julai mosi mwaka huu.
Tarimo amesema kuwa zoezi la kujisajili na utambuzi kwa wananchi Mkoani Morogoro litazinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera Agosti 4 mwaka huu lengo likiwa kila mwananchi ambaye ni Mtanzania halali aweze kupata kitambulisho cha Taifa.
Hatahivyo amesema kuwa ni jukumu la Maafisa watendaji wote kuhakikisha wananchi wamejiandikisha katika maeneo yao kwenye daftari la mkazi ili kurahisisha zoezi hilo litakapoanza pia amewataka kuacha kudai malipo yoyote kwani kazi hiyo ni wajibu wao.
Aidha Tarimo ameongeza kwa kusema kuwa hakuna mwananchi atakayepata Kitambulisho cha Taifa mpaka ajiandikishe kwenye daftari la mkazi katika eneo husika hivyo ni vyema kila mwananchi akajiandaa kuwa na vielelezo vya utambuzi kama vile kopi ya kitambulisho cha mpiga kura,cheti cha kuzaliwa,ubatizo, cheti cha ndoa,pasi ya kusafiria na vielelezo vingine ili iwe rahisi kutambulika pindi zoezi litakapoanza.
Zoezi la usajili na utambuzi kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa linaendeshwa na serikali kupitia mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambapo Kitaifa limeanzia Mkoani Dar es salaam na kwa Mkoa wa Morogoro litazinduliwa rasmi mapema mwezi ujao mwaka huu.

Tuesday, July 1, 2014

ANUSURIKA KUUWAWA BAADA YA KUKATAA UKEWENZA



Mkazi wa Mgeta aliyefahamika kwa jina la Faustina Selali 38 Mvomero mkoani hapa, yupo kwenye mateso makali akijiuguza kutokana na kipigo alichopata kutoka kwa mumewe wa ndoa aliyemtaja kwa jina la Lugasiani John Miasiku, kisa kikiwa ni mumewe huyo kutaka kuoa mke wa pili.
Mwanamke huyo amelazwa katika wodi nambi 3 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ambapo amesimulia kisa chote.

Akizungumza kwa tabu, Faustina amesema tukio hilo lililobadilisha historia ya maisha yake na kumwachia machungu moyoni mwake, lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa nne usiku ndani ya nyumba yao.
“Mimi na mume wangu tumeishi kwenye ndoa kwa muda wa miaka 20 na kufanikiwa kupata watoto watano. Kwa kipindi kirefu nilihisi ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, wakati naendelea kumchunguza, mume wangu akaniambia anataka kuoa mke wa pili,” alisema Faustina kwa uchungu na kuongeza:“Nikamhoji mume wangu, dini yetu hairuhusu jambo hilo na zaidi ya yote anachotafuta kwa huyo mke wa pili ni kitu gani wakati tayari mimi nimeshamzalia watoto watano na bado naendelea kuzaa?
“Hakuwa na jibu la maana, akaendelea kushikilia msimamo wake. Mwisho nikaona nisimlazimishe sana, nikamwambia kama hivyo ndivyo basi tugawane mali ili mimi niondoke aje huyo mwenzangu kwani sitakuwa tayari kuishi maisha ya uke wenza. Kwa kweli hakuwa na jibu la maana.”

“Ugomvi huo ulitokea Jumanne, kesho yake yaani Jumatano (siku ya tukio) mume wangu alivyorudi shamba nilimtengea ugali kama kawaida. Alikula vizuri tu tukapanda kitandani kulala, kama unavyojua tena wanandoa muda wao wa kuzungumza kwa utulivu ni usiku, nikaamua kuutumia muda huo kumwuliza mwenzangu.
“Nikamwambia kama bado ana msimamo wake uleule, anipe sehemu yangu niondoke zangu. Hapo nikawa nimechokoza moto. Ilikuwa ghafla tu, aliamka kitandani na kuchukua nyundo kisha akaileta kichwani na kunipiga nayo, baadaye akanipiga mdomoni na kuning’oa meno mawili ya mbele kwa kutumia ile nyundo.
“Hakuishia hapo, akanitoa panga kisha akanicharanga mikono yote, palepale damu zikaruka kama kachinja ng’ombe. Nilihisi maumivu makali sana, sikuwahi kupata maumivu makali kama yale. Kusema ukweli nilichanganyikiwa kabisa na kile kipigo.”


“Wakati akiendelea kunipiga bila huruma, alikuwa akisema dawa yangu mimi ni kufa ili aweze kumchukua huyo mwanamke wake bila usumbufu. Nilivyosikia hivyo ikabidi nitumie akili; nikajiangusha chini na kujifanya nimekata kauli ili nisiendelee kuumia.

“Alipoona hivyo kweli akaniacha. Akavaa nguo zake na kukimbia. Mwanangu mdogo Nesto akanisaidia kunikongoja hadi kwa jirani yetu Mzee Chota ambaye naye aliita majirani haraka, ilikuwa ni saa sita usiku, wakanikimbiza hadi Zahanati ya Mlali lakini nikapewa rufaa ya kuletwa hapa kutokana na hali yangu kuwa mbaya.”
Kwa mujibu wa Bi. Faustina, licha ya mume wake kumfanyia ukatili huo, ndugu wanaofika hospitalini hapo kumjulia hali, wanasema mumewe bado hajakamatwa na amekuwa akiendelea kutoa vitisho dhidi yake.
HABARI KWANZA lilifunga safari hadi kijijini Mgeta kwa lengo la kuhojiana na mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumkuta lakini alipomuona mwandishi wetu, Miasiku alitimua mbio akidhani alifuatwa na askari.

WAUGUZI WA HOSPITALI YA WILAYA YA KILOSA WATAKIWA KUWA NA LUGHA NZURI WANAPOWAHUDUMIA WAGONJWA HOSPITALINI HAPO.



 
Chama cha mapinduzi  CCM wilayani Kilosa mkoani Morogoro kimesikitishwa na hali inayojitokeza katika hospital ya wilaya kwa baadhi ya wauguzi wa afya kutoa lugha chafu  kwa wagonjwa mara wanapokwenda kupata matibabu hospitalin hapo.

Hayo yameelezwa na katibu waccm wilaya ya Kilosa Dodo Sambu hivi karibuni wakati wa kikao na mkurugenzi  wa halmashauri ya wilaya baada ya wazee hao kutoa malalamiko kuhusu wagonjwa kunyanyaswa na watoa huduma hao .

 Dodo ameeleza kuwa chama  cha mapinduzi kimepokea  kwa  masikitiko yanayotolowe na wananchi na wazee juu ya vitendo vya kutolewa lugha  chafu  vinavotendwa na watoa huduma hospitalini hapo.

Amesema kuwa  watoa huduma hao wa afya wanapaswa kuhudumia vizuri na  kwa upendo wagonjwa mara wanapofika kupata matibabu kwa kufuata maadili ya kazi zao.
Dodo ameongeza kuwa malamiko ambayo yanayotolewa kwenye kuwahudumia wagonjwa hospitalini hapo yanatendwa  na watoa huduma hao ambao wanasahau  kuwa waliapa kuwahidumia vizuri wagonjwa  hivyo  kufuatia hali hiyo chama cha mapinduzi wilaya kinaiomba halmashauri ya wilaya kuwachukulia hatua  wahudumu hao ikiwemo kupumzishwa kazi.