Mkazi wa Mgeta
aliyefahamika kwa jina la Faustina Selali 38 Mvomero
mkoani hapa, yupo kwenye mateso makali akijiuguza kutokana na kipigo alichopata
kutoka kwa mumewe wa ndoa aliyemtaja kwa jina la Lugasiani John Miasiku, kisa
kikiwa ni mumewe huyo kutaka kuoa mke wa pili.
Mwanamke huyo amelazwa katika wodi nambi 3 katika Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, ambapo amesimulia kisa chote.
Akizungumza kwa tabu, Faustina amesema tukio hilo
lililobadilisha historia ya maisha yake na kumwachia machungu moyoni mwake,
lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa nne usiku ndani ya nyumba yao.
“Mimi na mume wangu tumeishi kwenye
ndoa kwa muda wa miaka 20 na kufanikiwa kupata watoto watano. Kwa kipindi
kirefu nilihisi ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine, wakati
naendelea kumchunguza, mume wangu akaniambia anataka kuoa mke wa pili,” alisema
Faustina kwa uchungu na kuongeza:“Nikamhoji mume wangu, dini yetu hairuhusu
jambo hilo na zaidi ya yote anachotafuta kwa huyo mke wa pili ni kitu gani
wakati tayari mimi nimeshamzalia watoto watano na bado naendelea kuzaa?
“Hakuwa na jibu la maana, akaendelea
kushikilia msimamo wake. Mwisho nikaona nisimlazimishe sana, nikamwambia kama
hivyo ndivyo basi tugawane mali ili mimi niondoke aje huyo mwenzangu kwani
sitakuwa tayari kuishi maisha ya uke wenza. Kwa kweli hakuwa na jibu la maana.”
“Ugomvi huo ulitokea Jumanne, kesho
yake yaani Jumatano (siku ya tukio) mume wangu alivyorudi shamba nilimtengea
ugali kama kawaida. Alikula vizuri tu tukapanda
kitandani kulala, kama unavyojua tena wanandoa muda wao wa kuzungumza kwa
utulivu ni usiku, nikaamua kuutumia muda huo kumwuliza mwenzangu.
“Nikamwambia kama bado ana msimamo
wake uleule, anipe sehemu yangu niondoke zangu. Hapo nikawa nimechokoza moto.
Ilikuwa ghafla tu, aliamka kitandani na kuchukua nyundo kisha akaileta kichwani
na kunipiga nayo, baadaye akanipiga mdomoni na kuning’oa meno mawili ya mbele
kwa kutumia ile nyundo.
“Hakuishia hapo, akanitoa panga kisha akanicharanga mikono
yote, palepale damu zikaruka kama kachinja ng’ombe. Nilihisi maumivu makali
sana, sikuwahi kupata maumivu makali kama yale. Kusema ukweli nilichanganyikiwa
kabisa na kile kipigo.”
“Wakati akiendelea kunipiga bila huruma, alikuwa akisema
dawa yangu mimi ni kufa ili aweze kumchukua huyo mwanamke wake bila usumbufu.
Nilivyosikia hivyo ikabidi nitumie akili; nikajiangusha chini na kujifanya
nimekata kauli ili nisiendelee kuumia.
“Alipoona hivyo kweli akaniacha.
Akavaa nguo zake na kukimbia. Mwanangu mdogo Nesto akanisaidia kunikongoja hadi
kwa jirani yetu Mzee Chota ambaye naye aliita majirani haraka, ilikuwa ni saa
sita usiku, wakanikimbiza hadi Zahanati ya Mlali lakini nikapewa rufaa ya
kuletwa hapa kutokana na hali yangu kuwa mbaya.”
Kwa mujibu wa Bi. Faustina, licha ya mume wake kumfanyia
ukatili huo, ndugu wanaofika hospitalini hapo kumjulia hali, wanasema mumewe
bado hajakamatwa na amekuwa akiendelea kutoa vitisho dhidi yake.
HABARI KWANZA lilifunga safari hadi kijijini Mgeta kwa lengo la kuhojiana
na mtuhumiwa huyo na kufanikiwa kumkuta lakini alipomuona mwandishi wetu,
Miasiku alitimua mbio akidhani alifuatwa na askari.
No comments:
Post a Comment