Wakazi wa
Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wametakiwa kujiandaa na zoezi la usajili na
utambuzi kwenye daftari la wakazi katika maeneo yao wanayoishi ili kupata
kitambulisho cha Taifa ambacho ni muhimu kwa kila Mtanzania aliyefikisha umri
wa kuanzia miaka 18 na kuendelea.
Wito huo
umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Elias Tarimo ofisini kwake wakati
akizungumza kwenye kikao maalum kilichowahusisha Wakuu wote wa Idara na
Viongozi mbalimbali Julai mosi mwaka huu.
Tarimo
amesema kuwa zoezi la kujisajili na utambuzi kwa wananchi Mkoani Morogoro
litazinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera Agosti 4 mwaka huu
lengo likiwa kila mwananchi ambaye ni Mtanzania halali aweze kupata
kitambulisho cha Taifa.
Hatahivyo
amesema kuwa ni jukumu la Maafisa watendaji wote kuhakikisha wananchi
wamejiandikisha katika maeneo yao kwenye daftari la mkazi ili kurahisisha zoezi
hilo litakapoanza pia amewataka kuacha kudai malipo yoyote kwani kazi hiyo ni
wajibu wao.
Aidha Tarimo
ameongeza kwa kusema kuwa hakuna mwananchi atakayepata Kitambulisho cha Taifa
mpaka ajiandikishe kwenye daftari la mkazi katika eneo husika hivyo ni vyema
kila mwananchi akajiandaa kuwa na vielelezo vya utambuzi kama vile kopi ya
kitambulisho cha mpiga kura,cheti cha kuzaliwa,ubatizo, cheti cha ndoa,pasi ya
kusafiria na vielelezo vingine ili iwe rahisi kutambulika pindi zoezi
litakapoanza.
Zoezi la
usajili na utambuzi kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa linaendeshwa na
serikali kupitia mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambapo Kitaifa limeanzia
Mkoani Dar es salaam na kwa Mkoa wa Morogoro litazinduliwa rasmi mapema mwezi
ujao mwaka huu.
No comments:
Post a Comment