BAADHI YA MAJIMBO HAWA WAGOMBEA KWELI WAMECHUANA..
MATOKEO ya awali ya kura za urais, ubunge na udiwani yaliyoanza kutolewa jana kwenye vituo mbalimbali nchini, yameonyesha kuwa nyota ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, imeendelea kung’ara huku wagombea ubunge wa chama hicho nao wakionekana kufanya vizuri.
Habari kutoka Jimbo la Iringa Mjini, zinasema matokeo ya urais katika kata saba, mgombea wa urais wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alikuwa akiongoza dhidi ya mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Vituo hivyo ni stendi, Dk. Slaa (146), Kikwete (114), Ndiuka Dk. Slaa (133), Kikwete (272), Soko Kuu 2, Dk. Slaa (114), Kikwete (84), Zimamoto 1, Dk. Slaa (93), Kikwete (84), Zimamoto 2, Dk. Slaa (84), Kikwete (108), Hazina Dk. Slaa (138), Kikwete (97), IDYC Dk. Slaa (75) na Kikwete (72).
Katika Jimbo la Mbeya Mjini, matokeo ya ubunge vituo vya Block T- A, CHADEMA (140), CCM (33), kituo B, CHADEMA (115) na CCM (15).
Mbeya Mjini, katika Kata ya Mwakibete, Dk. Slaa (3,564), Kikwete (950), Kalobe Sekondari 1 Dk. Slaa (109), Kikwete (97), Kalobe Sekondari 2 Dk. Slaa (107), Kikwete (76), Kalobe Sekondari 5 Dk. Slaa (93) na Kikwete (85).
Geita kura za urais Kikwete (376), Dk. Slaa (341), kwa upande wa ubunge CCM (396), CHADEMA (322) na CUF (10) na kwa udiwani CCM (315), CHADEMA (474) na CUF (0).
Jimbo la Kyela matokeo ya urais katika kituo cha Nsesi, Kikwete 150, Slaa 119, kituo cha Katumba shuleni Kikwete 150, Slaa 120, Kilasilo, Slaa 36, Kikwete 205, Community Centre Slaa 125, Kikwete 56, Itungi Slaa 76, Kikwete 54. Katika kituo cha Bunge, jijini Dar es Salaam, Slaa 225, Kikwete 189.Arusha Mjini, katika Kata ya Kaloleni A1, Dk. Slaa amepata kura (112), Kikwete (59), Kaloleni A2, Dk. Slaa (119), Kikwete (76), Profesa Lipumba (2), Kaloleni A3, Dk. Slaa (104), Kikwete (61), Lipumba (1), Kaloleni A4, Dk. Slaa (109) na Kikwete (165).
Kituo B1, Dk. Slaa (118), Kikwete (67), Profesa Lipumba (0), kituo B2, Dk. Slaa (102), Kikwete 64, B3, Slaa 92, Kikwete 50, B4, Slaa 87, Kikwete (67) na Lipumba (3).
Jimbo la Segerea, Kata ya Kipawa, kituo Minazi mirefu A1 urais, Kikwete (79), Dk. Slaa (75), Profesa Lipumba (7), kituo A6, Dk. Slaa (69), Kikwete (62), kituo A2, Dk. Slaa (102), Kikwete (52), Profesa Lipumba (1), kituo B3, Kikwete (64), Dk. Slaa (78) na Profesa Lipumba (3).
Katika matokeo ya ubunge wa kata hiyo, mgombea wa CHADEMA, Godbels Lema alionekana akiongoza ambapo katika Kata ya Kaloleni A1, (113), dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Batilda Burian (54), Kaloleni A2, Lema (120), Burian (71), Kaloleni A3, Lema (109), Batilda (62), Kaloleni A4, Lema (111) na Batilda (63).
Jimbo la Ukerewe katika vituo vitatu, Mtoni, Nansio, Bwisya, mgombea wa CHADEMA, Salvatory Namuyaga wa CHADEMA alikuwa akiongoza akifuatiwa na mgombea wa CCM, Gertrude Mongela.
Katika Jimbo la Musoma Mjini, CHADEMA ilikuwa ikiongoza kwa madiwani katika kata nane, CCM ikipata kata tatu na CUF ikipata madiwani wawili.
Taarifa za awali zimedokeza kuwa Vincent Nyerere, alikuwa akiongoza kwa tofauti kubwa dhidi ya mgombea wa CCM, Vedasto Manyinyi.
Jimbo la Moshi Mjini, CHADEMA ilikuwa ikiongoza kwa kiti cha urais na ubunge huku upande wa madiwani ilikuwa ikiongoza kwa kupata viti 15 kati ya 21.
Hali hiyo, ilijitokeza katika majimbo ya Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini, ambako upinzani mkubwa ulikuwa kati ya vyama vya CCM na CHADEMA.
Katika Jimbo la Kigoma Mjini, Peter Serukamba wa CCM anachuana na Ally Mleh wa CHADEMA, huku katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wa CHADEMA anachuana na Robinson Lembo wa CCM.
Jimbo la Mbeya Mjini, mpaka tunakwenda mitamboni mgombea wa CHADEMA, Joseph Mbilinyi, ameonekana kuongoza dhidi ya mgombea wa CCM, Benson Mpesya.
Kituo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (DARUSO), urais Dk. Slaa (454), Kikwete (71), ubunge, John Mnyika wa CHADEMA (473) na Hawa Ng’umbi wa CCM (45).
Maswa, Magharibi, ubunge
Mgombea wa CHADEMA, John Shibuda, alikuwa akiongoza dhidi ya mgombea wa CCM, Peter Kisena, ambapo katika kituo cha Bukigi, Kata ya Malampaka Shibuda 113, Kisena 65, Sokoni Shibuda 68, Kisena 46, Sokoni B Shibuda, 61, Kisena 56, Mahakama A, Shibuda 66, Kisena 47, Mahakamani B, Shibuda 65, Kisena 50.
Shule ya Msingi Malampaka, Shibuda 54, Kisena 55, Chekechea A Shibuda 79 Kisena 5, Chekechea B, Shibuda 74, Kisena 53, Oil Mill, Shibuda 56, Kisena 36.
Jimbo la Nyamagana, inadaiwa mgombea wa ubunge Ezekiel Wenje, ameonekana kuongoza dhidi ya mgombea wa CCM, Lawrence Masha, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika jimbo hilo CHADEMA inaongoza kwa kupata madiwani katika kata 12 kati ya 14.
Katika Jimbo la Iringa Mjini, hadi tunakwenda mitamboni mgombea wa CHADEMA, Peter Msigwa, alikuwa akiongoza katika vituo vingi dhidi ya mgombea wa CCM, Monica Mbega.
DAR ES SALAAM NA MBEYA NAKO HALI ILIKUWA NI TETE
MASANDUKUKU TENA.?
ZOEZI la upigaji kura nchini limefanyika jana, huku zikiripotiwa kasoro kadhaa na baadhi ya watu wakikamatwa na kura za wizi pamoja na polisi kulazimika kupiga mabomu ya machozi.
Mjini Dar es Salaam, eneo la Mwananyamala Kisiwani, jana liligeuka uwanja wa vita, baada ya askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), kulazimika kupiga mabomu ya machozi kwa ajili ya kutawanya mamia ya wananchi waliokuwa karibu na eneo hilo.
Tuki hilo lilitokea majira ya saa 8:40 mchana baada ya wananchi kutilia shaka moja ya gari la waangalizi lililofika eneo hilo, wakidai lina boksi la kura zilizopigwa.
Tukio hilo, lilionekana kutaka kuvunja amani, hali iliyosababisha askari kupiga mabomu kwa lengo la kutawanya mamia ya wananchi walioonekana wakiwa wamejawa na hasira.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, mmoja wa maofisa waliokuwepo eneo hilo, alilazimika kuomba msaada wa askari zaidi ambao walifika wakiwa kwenye magari ya PT 2061, PT 0886 na PT 1523, likiwamo gari la kurusha maji ya kuwasha.
Kuwasili kwa magari hayo kulionekana wazi kupunguza kasi ya wananchi ambao awali walirusha mawe bila kujali kitu chochote kilichokuwa mbele yao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Elias Kalinga, aliyefika eneo hilo aliwaambia waandishi wa habari kuwa mbali na tukio hilo, hali ilikuwa shwari karibu katika vituo vyote.
“Ni kweli hapa kumetokea tukio hili, lakini kama mnavyoona hali imetulia, wananchi na kazi zinaendelea kama kawaida... maeneo yote yako shwari jamani kama mlivyoona,” alisema Kamanda Kalinga.
Katika tukio mbalo linaonekana kushtua watu wengi, ni pale mwanamke mmoja alikamatwa akiwa na mfuko wa rambo uliojaa kura zinazodaiwa kupigiwa mgombea mmoja wa urais huku akiwa kibindoni na sh 600,000.
Mwanamke huyo ambaye aligoma kutaja jina lake, alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi Minazini kabla ya kuchukuliwa na kuhamishiwa Kituo cha Polisi Oysterbay.
Kamanda Kalinga alipoulizwa na waandishi wa habari alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi leo baada ya uchunguzi kukamilika.
Katika tukio jingine, ni pale lilipowasili gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aina ya IVECO lenye namba za usajili 9003 JW 09 katika eneo hilo, hali iliyosababisha wananchi wengi kupigwa butwaa.
Lakini katika maeneo ya Kawe, Manzese, Sinza, Kigogo, Buguruni, TAZARA, Kinondoni, Msasani, Bunju, Ukonga, Kimara hadi jana jioni hali ilikuwa ni shwari.
Moja ya malalamiko makubwa katika maeneo mengi lilikuwa ni ukosefu wa majina mengi ya wapiga kura licha ya kuwa na shahada.
Mkoani Mbeya, kabla zoezi la kupiga kura, kulibainika kuwepo kwa njama za wizi wa kura baada ya kukamatwa kwa masanduku ya kupigia kura yakiwa na karatasi za kupigia kura kwa nafasi ya ubunge na urais.
Masanduku hayo yalikutwa juzi usiku nyumbani kwa msimamizi wa kituo cha Makole ambaye ni mwalimu, Wabuga Tarimo ambaye alitakiwa kuwa kituoni kwake kwenye kata hiyo, lakini alikiuka sheria na maagizo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuondoka na masanduku hayo yakiwa na karatasi za kupigia kura.
Baada ya wapiga kura kubaini njama hizo, huku wakidai wana haki ya kufahamu chimbuko la tukio hilo, wamelazimika kuweka ulinzi katika nyumba hiyo na kutoa taarifa kituo cha polisi ili kukamata vifaa hivyo.
Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Wilaya ya Dodoma, Jonathan Shani, alifika eneo la tukio na kuendesha upekuzi, alibaini uwepo wa masanduku hayo ambayo yalikuwa na karatasi za kupigia kura ambazo zilikuwa za wagombea ubunge na urais.
Kamanda huyo akiwa na mashuhuda walifungua masanduku na kubaini kuwa kura hizo bado hazijawekewa tiki.
Tukio hilo, liliwashutua wapiga kura wengi ambao walieleza hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa ni dalili tosha za kufanya njama za kuiba kura, jambo ambalo linaweza kuathiri matokeo ya kweli.
Baada ya kufanikiwa kuyakamata masanduku yao ambayo yalikuwa nyumbani kwa msimamizi huyo, kinyume cha utaratibu alipelekwa moja kwa moja kituo cha polisi ili kuhojiwa kwa lengo la kutaka kujua sababu za kuweka vifaa hivyo nyumbani kwake.
Akiwa chini ya ulinzi uliokuwa ukiongozwa na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Wilaya ya Dodoma Mjini, mtuhumiwa huyo, alidai alilazimika kwenda na vifaa hivyo nyumbani kwake kwa kuwa kituo cha kupigia kura kilikuwa mbali na hakuwa na ulinzi wowote.
Pamoja na tukio hilo kushuhudiwa na Kamanda wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma Zelote Stephen, alipohojiwa kuhusu suala hilo alisema hajapata taarifa zozote.
KONDOA NAKO
Vibanda vya kupigia kura katika Wilaya ya Kondoa vimechomwa moto na watu wasiojulikana na kusababisha wasimaamizi na wapiga kura kuendesha shughuli zao katika mazingira ya jua kali.
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Zelote Stephen, na kudai kuwa vibanda hivyo viliunguzwa na watu wasiojulikana, japo hakuna hasara yoyote iliyotokea.
NAKO KAWE
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia na baadhi ya wananchi, wameshindwa kupiga kura baada ya majina yao kukosekana katika vituo walivyojiandikishia.
Hali hiyo ilijitokeza jana majira ya saa 2 asubuhi, baada ya mgombea huyo kufika katika kituo namba tatu cha Sokoni Juu, kwa ajili ya kupiga kura, lakini jina lake lilikosekana katika daftari la wapiga kura.
Akizungumzia kitendo hicho, Mbatia alisema watu wengi watapoteza haki zao kutokana na kushindwa kupata majina yao.
“Wakati wa zoezi la kuhakiki majina nilifika ili kuangalia jina langu…nilipolikosa nilifanya mawasiliano ili kujua lililojitokeza huku nikiwa na shahada yangu namba 17460120 lakini NEC ilidai kulijishughulikia suala hilo,” alisema Mbatia.
HUKO KASURU VIJIJINI NAKO.Wananachi wa kata za Nyachenda na Kitagata, zilizopo Jimbo la Kasulu Vijijini, wameshindwa kupiga kura za udiwani kutokana na kutokuwapo kwa karatasi za kupigia kura na kifo cha mgombea.
Mratibu wa uchaguzi mkoani Kigoma, Anthony Jakonyango, alisema katika Kata ya Kitagata uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana na kutokuwepo kwa karatasi za kupigia kura.
Wakati Kata ya Nyachenda uchaguzi haukuweza kufanyika kutokana na kifo cha mgombea udiwani wa kata hiyo, kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Bernard Machupa, aliyefariki dunia wiki tatu zilizopita.
Alisema mpaka sasa haijafahamika wananchi hao watapiga lini kura, kwani tume bado haijapanga tarehe ya uchaguzi.
Mbali na kasoro hizo, uchaguzi mkoani Kigoma umefanyika kwa amani na watu walianza kujitokeza vituoni tangu saa 12:30 asubuhi kabla ya muda wa kufungua vituo.
Katika Jimbo la Kigoma Mjini, Peter Serukamba wa CCM anachuana na Ally Mleh (CHADEMA), huku katika Jimbo la Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe wa CHADEMA anachuana na Robinson Lembo wa CCM.
HUKO MBEYA MJINI
Hali ilikuwa tete katika kituo cha Mzalendo, jimboni hapa, baada ya wananchi kutishia kutopiga kura kutokana na wasimamizi wa kituo hicho kuingia kwenye chumba cha kupigia kura wakiwa na makoti makubwa na mabegi, hali iliyowapa wasiwasi wapiga kura.
Kutokana na hali hiyo, wananchi waliwataka wasimamizi kuvua makoti waliyovaa pamoja na mabeki na kuwataka wayatoe nje kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza, jambo ambalo wasimamizi hao walilitii na kuruhusu upigaji kura kuendelea.
Hata hivyo, wananchi hao walieleza kasoro nyingine katika kituo hicho kuwa ni kutokuwepo kwa askari wa kusimamia kituo, hali ambayo iliwatia wasiwasi endapo kungetokea vurugu.
HUKO ARUSHA
Mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha kwa tiketi ya CHADEMA, Godbles Lema, amejeruhiwa kwa jiwe katika mguu wake wa kushoto na kada wa CCM anayefahamika kwa jina la Musa Abdallah, ambaye hivi sasa anashikiliwa na polisi.
Mbali na tukio hilo, daftari la wapiga kura katika Kata ya Sombetini lenye majina 470 limeibwa jana majira ya saa 3:30 asubuhi katika mazingira ya kutatanisha.
Kutokana na matukio hayo, msimamizi wa kituo hicho, Charles Munis, anashikiliwa na polisi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Basilio Matei, amethibitisha kutokea kwa matukio hayo.
Taarifa hii imeandaliwa na Danson Kaijage (Dodoma), Iddi Risasi (Kigoma), Christopher Nyenyembe na Mosses Ng’wat (Mbeya), Grace Macha (Moshi), Ramadhani Siwayombe (Arusha), Neema Kishebuka (Tanga) na Betty Kangonga (Dar).
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuahirisha uchaguzi katika majimbo matatu na kata 23 kutokana na upungufu wa karatasi za kupigia kura.
Mkurugenzi wa NEC, Rajab Kiravu aliyataja majimbo hayo jana kuwa ni Nkenge, Mpanda Mjini na Mpanda Vijijini.
Alisema katika majimbo hayo matatu ambayo uchaguzi umeahirishwa wapiga kura wataendelea kupiga kura ya rais na madiwani kama ulivyopangwa.
Aidha, alizitaja kata ambazo zimesimamishwa uchaguzi wake ni Endegikot iliyopo Mbulu, Mbede iliyopo Mpanda, Kisiwani iliyopo Same na Kata ya Matonya iliyopo Newala.
Kata nyingine ni Mji Mwema iliyopo Njombe, Kigwa na Ibelamikundi zilizopo Uyui, Kata za Gongo la Mboto iliyopo Ilala, Msogezi iliyopo Ulanga, Kimuli na Kamuli zilizopo Karagwe.
Kata za Kisanga iliyopo Sikonge, Mkuyuni na Mirongo za Mwanza, Kitagata iliyopo Kasulu, Buseresere iliyopo Chato na Mazinga iliyopo Muleba.
Mkurugenzi huyo alisema kata nyingine ni Kilangalanga iliyopo Kibaha na Kibiti, Chemchem, Ngorongo, Kipungira na Mjawa zilizopo Rufiji.
“Katika Kata ambazo uchaguzi wa madiwani umehairishwa uchaguzi wa rais na wabunge utaendelea kufanyika kama ulivyopangwa awali,” alisema Kiravu.
Alisema tume itatangaza baadye siku za kufanyika kwa chaguzi hizo zilizoahirishwa.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, mgombea ubunge wa Mpanda Kati kwa tiketi ya chadema, Said Arfi, alisema hadi majira ya saa nane mchana jana hakuwa na barua rasmi ya kusimamishwa kwa uchaguzi huo.
Hata hivyo, alisema alishangaa asubuhi kusikia redioni na kwamba hakuwa na taarifa zozote za kutofanyika kwa uchaguzi jimboni hapo.