Wednesday, November 24, 2010

FINCA TANZANIA WAWASHAURI WANANCHI KUTOJISAAHAU NA MIKOPO WANAYOPATA

FINCA TANZANIA WAWASHAURI WANANCHI KUTOJISAAHAU
NA MIKOPO WANAYOPATA

Wafanyabiashara mbalimbali wilayani Njombe Mkoani Iringa wametakiwa kutojisahau pindi wanapopata mikopo kwenye mashirika mbalimbali yanayotoa mikopo hiyo ili kuboresha biashara zao na kujikwamua na umaskini.

Hayo yamesemwa na Meneja wa shirika la mikopo la FINCA TANZANIA LIMITED tawi la Njombe Bwana Binnah Wakibara wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Bwana Wakibara amesema kuwa shirika lake linatoa mikopo kwa njia mbili ambapo ni kupitia vikundi au mtu binafsi na kuongeza kuwa mkopo huo ni kwa ajili ya kuendeleza na kukuza biashara na siyo kuanzishia au kufanyia shughuli nyingine tofauti.

Akieleza changamoto walizokutana nazo tangu kuanzishwa kwa tawi hilo mjini Njombe mwaka 2005,amesema kuwa baadhi ya watu waliofanikiwa kuchukua mikopo hiyo wamekuwa wakishindwa kulipa marejesho katika wakati unaotakiwa kutokana na kuyumba kwa biashara zao au baadhi ya wateja kuchukua mikopo binafsi ambapo hushindwa kurejesha kwa wakati.

Aidha amewataka wananchi wa Njombe ambao ni wajasiliamali kutoogopa kufika ofisini kupata maelezo namna ya kupata mkopo huo na kuongeza kuwa FINCA ni kwa ajili ya kukuza kipato cha mfanyabiashara na kwamba masharti ya mikopo hiyo ni nafuu.

No comments:

Post a Comment