Friday, November 26, 2010

NJAA YASUMBUA WAKAZI WAKATA YA NDULI MKOANI IRINGA.

WALIHAIDIWA KUPEWA CHAKULA CHA
MSAADA NA WAGOMBEA WAO.

Wananchi wa kata mpya ya Nduli katika Manispaa ya Iringa wameomba kupatiwa chakula cha msaada kutokana na njaa kali inayowakabili kwa madai kuwa tangu waiombe serikali iwapatie msaada huo, hawajawahi kusaidiwa.

Imedaiwa kuwa Wananchi hao wamekuwa wakila mlo mmoja kwa siku na wanafunzi wa shule za msingi wameathirika zaidi kwa kuwa shule nyingi hazina uwezo wa kuwaandalia wanafunzi chakula cha mchana hali inayopelekea kutokuwa na isikivu wa kutosha wanapokuwa darasani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nduli, Ayubu Mwenda alisema tatizo la chakula limekuwa kubwa, kutokana na mazao mengi kukauka kabla ya kukomaa kufuatia ukame ulioathiri kata yao.

Amesema tatizo hilo, limeshusha kwa kiasi kikubwa kiwango cha wanafunzi kufaulu kwa madai kuwa wengi wao wamekuwa wakienda shule bila kula chochote hadi jioni wanaporejea nyumbani.

Wananachi hao walisema kuwa wakati wa kampeni, waliahidiwa kupewa chakula na wagombea wao, lakini bado hawajakumbukwa jambo ambalo linawafanya waanze kukosa imani na viongozi waliowaweka madarakani.

Kwa upande wake diwani mpya wa Kata ya Nduli, aliahidi kutoa chakula cha msaada kwa ajili ya wanafunzi wa maeneo ya kata hiyo mara shule itakapofunguliwa na kwamba hivi sasa hawezi kutokana na ukweli kwamba bado hawajaanza kazi.

Takwimu za awali zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wakati kata hiyo haijahamishiwa katika Halmshauri ya Manispaa, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 13,000 wanakabiliwa na tatizo la njaa katika kata hiyo.

No comments:

Post a Comment