Sunday, March 17, 2013

TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI KUIWINDA MOROCCO

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 17, 2013

TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI KUIWINDA MOROCCO

Taifa Stars imeanza kambi jana jioni (Machi 16 mwaka huu) ambapo wachezaji 14 kati ya 23 walioitwa wameripoti na kufanya mazoezi leo asubuhi chini ya Kocha Kim Poulsen.

Wachezaji walioripoti ni nahodha Juma Kaseja kutoka Simba na msaidizi wake Aggrey Morris wa Azam, Erasto Nyoni (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba), Shomari Kapombe (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Wengine ni Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Mrisho Ngasa (Simba) na Simon Msuva (Yanga).

Wachezaji Hussein Shariff, Issa Rashid na Shabani Nditi ambao timu yao ya Mtibwa Sugar jana ilicheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mjini Turiani wataripoti kambini leo jioni.

Kikosi hicho kitakamilika Jumanne asubuhi baada ya wachezaji walio katika kikosi cha Azam nchini Liberia kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho kurejea nchini. Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo (DRC) wanatarajiwa kutua nchini kesho usiku.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

MECHI YA RUVU SHOOTING, YANGA YAINGIZA MIL 62/-

MECHI YA RUVU SHOOTING, YANGA YAINGIZA MIL 62/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting na Yanga iliyochezwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 62,228,000 kutokana na watazamaji 10,929.

Viingilio katika mechi hiyo namba 146 iliyomalizika kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 14,336,764.95 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 9,492,406.78.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,289,880.48, tiketi sh. 4,136,390, gharama za mechi sh. 4,373,928.29, Kamati ya Ligi sh. 4,373,928.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,186,964.14, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) sh. 850,486.06 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 850,486.06.

WAANGOLA KUCHEZESHA MECHI YA STARS

WAANGOLA KUCHEZESHA MECHI YA STARS

Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limeteua waamuzi kutoka Angola kuchezesha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco (Lions of the Atlas).

Mechi hiyo ya kundi C itachezwa Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast ndiyo inayoongoza kundi hilo ikiwa na pointi nne na kufuatiwa na Taifa Stars yenye pointi tatu.

Mwamuzi wa mechi hiyo ni Helder Martins de Carvalho wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Inacio Manuel Candido huku Ricardo Daniel Cachicumi akiwa mwamuzi msaidizi namba mbili. Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Antonio Muachihuissa Caxala.

Waamuzi hao watawasili nchini saa 1.20 usiku Machi 22 mwaka huu kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Luanda, Angola kupitia Nairobi, Kenya.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa David Fani kutoka Botswana anatarajiwa kuwasili Machi 22 mwaka huu saa 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

Naye mtathmini wa waamuzi (referee assessor) Neermal Boodhoo kutoka Afrika Kusini atawasili nchini Machi 22 mwaka huu 1.45 usiku kwa ndege ya South African Airways.

Saturday, March 16, 2013

WATOTO WALEMAVU WA KITUO CHA BETHELEHEMU WILAYANI KILOMBERO WAPATIWA ZAWADI YA SIKUKU YA PASAKA

WATOTO WA KITUO CHA BETHELEHEMU KILOMBERO WAPATIWA ZAWADI YA SIKUKU YA PASAKA.

Wanawake wa kata ya Kibaoni Wilayani Kilombero wametoa msaada wa mbuzi wawili kwa ajili ya sikukuu ya pasaka kwa watoto walemavu wa akili wa kituo cha bethelehemu unaogharimu jumla ya shilingi 180,000.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Mratibu wa kamati ya sherehe ya siku ya mwanamke duniani Bi Sophia Msiku amesema kuwa msaaada huo umepatikana baada ya wanawake hao kufanya harambee katika sherehe ya siku ya wanawake duniani.

Bi Msiku amesema kuwa katika kusherekea siku ya mwanamke duniani walipanga kushiriki na watoto hao lakini kutokana na mambo kuingiliana walishindwa kufanya hivyo na badala yake walipanga siku ya kupeleka msaada huo.

Akizungumza wakati akipokea msaada huo mlezi mkuu wa kituo hicho Sister Maria Dorothea Lyimo amewashukuru akina mama hao na amewataka watu wengine kuiga mfano huo kwa kutoa msaada huo kwa watoto hao .

Tuesday, March 12, 2013

WAKULIMA WILAYANI KILOMBERO WALALAMIKIA UCHELEWESHWAJI WA MBOLEA ZA RUZUKU

WAKULIMA WILAYANI KILOMBERO WALALAMIKIA UCHELEWESHWAJI WA MBOLEA ZA RUZUKU .

Wakulima wa vitongoji vya lipangalala,lihami,kwa mkuya na kiyongwile kata ya Ifakara Wilayani Kilombero wamelalamikia kucheleweshwa mbolea ya ruzuku  ambayo ilitakiwa kufika tangu mwezi wa kumi na mbili mwaka jana.

Wakizungumza na Mtandao huu wa habarikwanza Baadhi ya wakulima wamesema kuwa pembejeo katika maeneo hayo zimechelewa kufika hali ambayo imewafanya wakulima hao kushindwa kuzitumia hasa zile za kupandia kutokana na muda kupita.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya kugawa vocha za pembejeo katika maeneo hayo Bwana Paulo Magehema amekiri malalamiko ya wakulima hao ambapo amesema kuwa mbolea hiyo ilitakiwa ifike mwaka jana lakini imefika mwezi machi mwaka huu  huku  mimea ikiwa imeshaota na kukua hivyo kwa upande wa mbolea ya kupandia haitafanya kazi yoyote.

Hata hivyo amesema pamoja na kucheleweshwa kwa mbolea hizo wakulima 300 watanufaika na mbolea hizo ambazo zimefika  chache ambazo hazitakidhi idadi ya wakulima waliotuma maombi ya kupatiwa mbolea hizo




WANAFUNZI WILAYANI KILOMBERO WAHIMIZWA KUONGEZA BIDII KATIKA MASOMO YAO KUEPUKA AIBU YA MATOKEO KATIKA MITIHANI YAO YA KUHITIMU

WANAFUNZI WILAYANI KILOMBERO WAHIMIZWA KUONGEZA BIDII KATIKA MASOMO YAO

Wanafunzi wilayani Kilombero wamehimizwa kuongeza bidii katika masomo ili wafanye  vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne na kuondokana na aibu ambayo taifa imepata  kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne  kwa mwaka 2012 kufeli.

Hayo yameelezwa leo na mbunge wa jimbo la Kilombero Mheshimiwa Abdul Mteketa wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kata ya Kibaoni alipokuwa akitoa msaada wa vitabu 100 vya masomo ya hesabu,jiografia,kemia,fizikia na bailojia katika shule hiyo.

Mh,Mteketa amesema kuwa kufeli kwa wanafunzi wengi inatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vitabu ,walimu na baadhi ya wanafunzi kutokuwa na nidhamu hivyo amewataka   wazazi ,walezi na walimu kushirikiana  kikamilifu ili kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo .

Kuhusu baadhi ya wanafunzi kutokuwa na nidhamu kwa walimu na utoro,amesema suala la nidhamu kwa mwanafunzi ni ushirikiano kati ya wazazi na walimu na hivyo amewataka wazazi kuwa wakali kwa watoto wao pindi wanapokosea  badala ya kuwatetea , hali hiyo inasababisha wanafunzi wengi kutokuwa na nidhamu pindi wanapoona wanatetewa na wazazi wao.

Awali akizungumza wakati akipokea msaada huo kwa niaba ya shule mkuu wa shule hiyo  Bwana Zakaria Kalinga amemshukuru Mh Mteketa  kwa msaada wa vitabu 100 na amemuomba asichoke kuitembelea shule hiyo na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo.

Bwana Kalinga amesema shle hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitabu,uchache wa samani za ofisi,uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi,ukosefu wa nyumba za walimu,ukosefu wa hostel na ukosefu wa vifaa vya michezo na fedha kwa ajili ya matengenezo ya uwanja .

Kuhusu vifaa vya michezo na matengenezo ya uwanja mbunge huyo  amewaahidi atahakikisha anatekeleza ahadi hiyo.

Monday, March 11, 2013

MBUNGE WA JIMBO LA KILOMBERO MH.ABDUL MTEKETA ATOA MSAADA WA VITABU 200 VYA MASOMO MBALIMBALI KATIKA SHULE YA SEKONDARI KIYONGWILE

MBUNGE WA JIMBO LA KILOMBERO MH.ABDUL MTEKETA ATOA  VITABU 200 VYA MASOMO MBALIMBALI KATIKA SHULE YA SEKONDARI KIYONGWILE

MBUNGE wa Jimbo la Kilombero Mheshimikwa Abdul Mteketa ametoa msaada wa Vitabu 200 vya Masomo mbalimbali kwa Shule ya Sekondari ya Kiyongwile iliyopo Kata ya Ifakara.

Akizungumza na Wanafunzi na Walimu wa Shule  hiyo Wakati akikabidhi msaada huo Mheshimiwa Mteketa amewaeleza kuwa  Lengo  la msaada huo ni kuinua Taaluma na kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi  wa shule hiyo na pia ni moja ya kutekeleza ahadi ya kuboresha Elimu kwa shule za Msingi na Sekondari katika Jimbo la Kilombero.

Amewataka Wanafunzi na Walimu kuvitunza Vitabu hivyo ili Viwasaidie wanafunzi waliopo kwa sasa na watakaokuja baadaye.
Msaada uliotolewa ni Vitabu vya Masomo ya Fizikia, Kemia, Jiografia, Baiolojia na Hisabati.

Mbali na Msaada huo Mbunge huyo ametoa Msaada wa Kalamu za Wino na Mkaa zenye Thamani ya Shilingi Laki Moja na Elfu Hamsini (150,000/=)kwa shule ya Msingi ya Lipangalala huku akiwaahidi kujenga Vyoo na kuweka Maji katika Shule hiyo.

Mheshimiwa Mteketa ametoa ahadi hiyo baada ya uongozi wa shule hiyo kumweleza matatizo hayo likiwemo  na tatizo la Ukosefu wa Umeme shuleni hapo.










KILOMBERO PLANTATION LIMITED YATOA MSAADA WA PIKIPIKI KWA JESHI LA POLIS WILAYANI KILOMBERO YENYE THAMANI YA TSH M 1.75

KILOMBERO PLANTATION LIMITED YATOA  PIKIPIKI KWA JESHI LA POLISI WILAYANI KILOMBERO YENYE THAMANI YA TSH M 1.75 
 
Kituo Kidogo cha Polisi cha Mngeta kilichopo wilayani Kilombero kimepatiwa msaada wa pikipipiki moja aina ya bajaji Boxer yenye thamani ya shilingi 1,750,000 kutoka kampuni ya Kilombero Plantation Limited KPL.

Meneja Rasilimali watu wa kampuni hiyo Bwana David Lukindo amesema kuwa msaada huo umekabidhiwa hivi karibuni na mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo Bwana Cater Coleman.

Bwana Lukindo amesema kuwa kampuni imetoa msaada huo baada ya kutambua kituo hicho kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa usafiri na msaada huo na anaamini kwa kiasi kidogo watakuwa wamesaidia katika kuimarisha ulinzi katika tarafa ya mngeta.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa msaada wa pikipiki hiyo Mkuu wa kituo hicho Mkaguzi msaidizi wa Polisi Joseph Elias,ameishukuru kampuni hiyo kwa msaada huo na anawaomba wadau wengine kuiga mfano wa KPL.

Bwana Elias amesema kuwa jeshi la polisi linakabiliwa na changamoto nyingi hususan usafiri hali inayowafanya kushindwa kuwafikia wananchi katika maeneo mengi hivyo kupatikana kwa  usafiri huo utasaidia jeshi hilo kupambana na wahalifu kwa kuwafikia wananchi wengi ,ili kupunguza vitendo vya uhalifu katika tarafa ya mngeta.
 

Friday, March 8, 2013

WAKANDARASI WAASWA KUFANYA KAZI ZAO KATIKA KIWANGO KINACHOSTAHILI.

WAKANDARASI WAASWA WILAYANI KILOMBERO

WAKANDARASI wa Ujenzi Nchini wametakiwa kufanya Kazi  zao kwa kuzingatia Sheria, ubora na Kiwango cha Hali ya Juu.

Akiongea mara baada ya kukagua maandalizi ya Awali ya Ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero Mkoani Morogoro, Naibu Waziri wa Ujenzi Injinia Greyson Lwenge amesema kuwa ubora wa hali ya juu unahitajika katika ujenzi unaofanyika na makandarasi wakabidhi Daraja likiwa katika kiwango cha juu.

Amesema kuwa jumla ya fedha Shilingi Bilioni 53 zitatumika katika kukamilisha Ujenzi wa Daraja hilo litakalokamilika Januari 2015.

Tayari shilingi Bilioni 8 zimekwishatolewa kwa ajili ya Mandalizi ya Awali ya Ujenzi wa Daraja hilo linalounganisha Wilaya ya Kilombero na Ulanga.
 Kivuko katika mto kilombero kikitumika kuvusha abiria,wakati wakazi wake wakisubiri    kumalizika kwa daraja mwaka 2015. (picha na Henry Bernard Mwakifuna.)


Awali Injinia Mkuu wa Kampuni ya China Railways Group wanaojenga Daraja hilo Liang Yan Ping amesema kuwa watajenga Daraja hilo kwa Kiwango kwa kuwa wanauzoefu wa Ujenzi wa madaraja.

Liang amesema kuwa Muda wa Miezi 24 uliowekwa utatumika kukamilisha ujenzi huo, ingawa wako Nyuma katika Miezi Mitatu waliopewa kwa ajili ya Maandalizi ya Ujenzi huo.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Ujenzi Injinia Greyson Lwenge amesema kuwa Barabara ya Mikumi, Ifakara, Lupiro hadi Lumecha Mkoani Ruvuma ipo kwenye mchakato wa kupata Wakandarasi watakaoiwekea Lami.

Amesema kuwa Barabara hiyo yenye Urefu wa Kilomita 512 ni muhimu kwa Mkoa wa Morogoro na Taifa kwa Ujumla inataraji kuwa katika Kiwango kizuri ifikapo Mwaka 2015.

Thursday, March 7, 2013

MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KILOMBERO BI AZIMINA MBILINYI KUONGOZA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI WILAYANI HUMO.



SIKU YA MWANAMKE DUNIANI


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Bi Azimina Mbilinyi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ambayo yataadhimishwa na wanawake wa  kata ya Kibaoni katika viwanja vya soko la Kibaoni.

Mratibu wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo Bi Sophia Msiku ambae ni Afisa Mtendaji wa kata hiyo amesema kuwa kata ya kibaoni imejipanga vizuri katika maadhimisho hayo .

Bi Msiku  amesema kuwa maadhimisho hayo yataanza kwa maandamano kuanzia maendeeleo na maandamano hayo yatapokelewa na Mgeni rasmi katika viwanja hivyo.

Amesema katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho ya sanaa,michezo mbalimbali,na pia wanawake watatoa ushuhuda mbalimbali.

Ameongeza kuwa Mbali na kutoa ushuhuda mbalimbali pia  elimu ya watu kujua haki zao katika kupambana na rushwa itatolewa
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema kuwa uelewa wa masuala ya jinsia katika jamii,ongeza kasi.




SERIKALI YA KIJIJI CHA MCHOMBE YAHUSIKA NA UPOTEVU WA FEDHA JUMLA YA MILIONI 2.19

WANANCHI WA KIJIJI CHA MCHOMBE WAWAONDOA VIONGOZI WAO  WA SERIKALI MADARAKANI.


Wananchi wa Kijiji cha Mchombe wamewaondoa madarakani viongozi wa serikali ya kijiji hicho  katika mkutano wa kijiji kutokana na kuhusika na upotevu wa fedha jumla ya shilingi 2,190,000.

Kaimu Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mngeta Bwana Shabani Mgaya amesema kuwa Kuondolewa madarakani kwa serikali hiyo kumetokana na taarifa ya mkaguzi wa ndani wa hesabu za serikali kubaini  makosa mbalimbali yaliyofanywa na serikali hiyo.

Amesema serikali hiyo imefanya upotevu wa shilingi 2,190,000 ambazo zimepotea kwa uzembe wa viongozi hao ambapo shilingi 1,780,000 ilitolewa benki na ilitumika bila ya idhini ya serikali.

Aidha Bwana Mgaya amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi imeeleza kuwa kati ya fedha hizo shilingi 300,000  zilitokana na uuzwaji wa ardhi ya kijiji ambapo ni kinyume na sheria kwani ardhi hiyo iliuzwa bila ya kufuata taratibu na pesa hiyo haikuonekana.

 Taarifa hiyo ya mkaguzi ambayo imewafanya wananchi kuuondoa uongozi madarakani imeeleza kuwa shilingi 1,100,000 fedha kutoka mfuko wa jimbo ambayo ilikuwa kwa ajili ya uchimbaji wa visima imetumika kwa matumizi mengine tofauti na yaliyokusudiwa.

 Aidha miongoni mwa mambo yaliyobainika katika taarifa ya  mkaguzi wa ndani kwa viongozi wa serikali hiyo ni udhaifu wa serikali katika kukusanya mapato,udhaifu wa kutosimamia shughuli za maendeleo na kutosoma taarifa za mapato na matumizi kwa vipindi vitatu mfululizo.




Wednesday, March 6, 2013

MAZISHI YA MWIGIZAJI ALIYEPOTEA MKOANI NJOMBE YAFANYIKA.

Mazishi ya Mkazi Mmoja wa Kibena Mjini Njombe bwana Mexon Nyekelela Chota Yamefanyika Katika Makaburi ya Kibena,Ikiwa ni Baada ya Kupatikana Kwa Mwili wa Marehemu Uliokuwa Amezama Kwa Siku ya Tano Katika Mabwawa ya Kampuni ya TANWAT Mjini Njombe.

Akizungumza Mara Baada ya Kupatikana Kwa Mwili Huo Afisa Tarafa ya Njombe Mjini Bi Lilian Nyemele Ameishukuru Kampuni ya TANWAT Kwa Namna Ilivyoshiriki Katika Kusaidia Zoezi Hilo Pamoja na Wananchi Wote Walioshiriki.





Mwili wa Marehemu Ulipatikana Leo Majira ya Saa Nane Mchana Ikiwa ni Baada ya Jitihada za Muda Mrefu za Wananchi na Viongozi Kuweza Kuutafuta Mwili Huo Bila Mafanikio Kutokana na Ukosefu wa Vifaa Vya Uokozi.

Akizungumza Mara Baada ya Kuwasili Mkoani Njombe Mtaalam wa Uzamiaji Kutoka Jijini Dar Joseph Mapunda Anasema Kuna Haja Kwa Serikali ya Mkoa wa Njombe Kuanza Kutoa Mafunzo Kwa Wananchi na Wataalam Mbalimbali Ili Kuweza Kupata Wataalam wa Uzamiaji.

Marehemu Mexon Nyekelela Chota Alizama Kwenye Mabwawa Hayo Mnamo March Mosi Mwaka Huu Majira ya Saa Kumi na Moja Jioni Wakati Akiwa na Wenzake Mara Baada ya Kumaliza Shughuli Zao za Sanaa.

Monday, March 4, 2013

PONGEZI KWA AZAM FC KUSONGA MBELE


Release No. 037
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 4, 2013

PONGEZI KWA AZAM KUSONGA MBELE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika.

Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi inayofuata.

Timu ya Azam inayofundishwa na Mwingereza John Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na jana kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.

Kwa kufanikiwa kuing’oa Al Nasir Juba, Azam sasa watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya michuano dhidi ya Barrack Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha suluhu katika mechi ya marudiano jijini Freetown.

Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi 15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

TIMU YA KIKAPU YA ST JOSEPH MOROGORO YACHAKAZWA 71-16

TIMU YA KIKAPU YA ST JOSEPH MOROGORO YACHAKAZWA 71-16.


Mchezaji wa timu ya Mt.Joseph Andrew,akijaribu kuokoa mpira katika mchezo uliofanyika juzi katika uwanja wa Polster Club dhidi ya Kihonda Hits(Picha na Mussa Enock)

Timu ya kikapu ya chuo cha Mtakatifu Joseph kilichopo kihonda barabara mpya Mkoani morogoro imechakazwa vibaya kwa jumla ya point/alama  71-16 dhidi ya timu ya Kihonda Hits katika mchezo wa kirafiki uliofanyika siku ya jumamosi ya tarehe 02 mwezi 03 mwaka huu.

Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Polister Club  uliopo Kihonda Maghorofani ulimalizika  kwa timu ya chuo cha Mtakatifu Joseph kwa kucharazwa jumla ya point/alama 71 kwa 16 dhidi ya wapinzani wao Kihonda Hits.

Mchezo huo ulioanza kwa kasi na kuwafanya timu ya Kihonda Hits kuanza kupata point/alama 6 mfululizo na katika dakika ya 8 ya mchezo mchezaji hatari wa  st joseph maarufu kwa jina la Kulwa aliweza kuwainua mashabiki wa timu ya Chuo cha Mtakatifu Joseph kwa kufunga point zililochochea kasi ya mchezo kuongezeka kwa timu hiyo.

Hata hivyo jitihada hizo hazikuleta matumaini ya kutosha kwa upande wa timu ya chuo cha  Makatifu Joseph kwani hadi timu zinaenda mapumziko matokeo yalikua ni 37-12,Matokeo ambayo yalianza kuwavunja moyo wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.