Afisa Elimu kutoka shirika la mkuhumi Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro Shadrack Yoash amewataka wakulima kuacha kulima kilimo cha mazoea na
kinachoathiriwa na mabadiliko ya tabia ya nchi na badala yake walime kilimo cha
kisasa ili waweze kuepukana na umasikini.
Hayo ameyasema julai 8 mwaka huu kwenye sherehe za wakulima
wa shamba darasa zilizofanyika katika kijiji cha Lunezi kitongoji cha Manyomvi
kata ya Lumuma Wilayani humo ambazo zimeandaliwa na Shirika lisilo la
kiserikali Mkuhumi.
Yoash amesema kuwa mabadiliko ya tabia ya nchi yalivyo na
kasi kwa kipindi hiki huku wananchi wakiendelea kulima kilimo cha mazoea
hawataweza kupata mavuno ya kutosha na kwamba watazidi kukata misitu kwa ajili
ya kuongeza mashamba hali itakayo sababisha kutokea kwa ukame na hatimaye
wakulima kuwa na kipato kidogo na kushindwa kumudu familia zao.
Ameongeza kwa kusema kuwa
shirika la Mkuhumi umeanzisha rasmi shamba Darasa tangu Mwaka 2010
katika vijiji 8 Wilaya ya Kilosa na kwamba kila Kijiji kuna vikundi viwili vinavyotekeleza mradi wa
shamba darasa na kwamba wameanzisha mfumo wa kutoa zawadi kwa kila kikundi
kinachofanya vizuri na mkulima mmoja mmoja kama motisha ili waweze kufanya
vizuri.
Katika sherehe hizo ambapo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa
Halmashauri wilaya ya Kilosa Amer Mubarak ameweza kukabidhi zawadi kwa mshindi
wa kwanza hadi wa tatu pamoja na kikundi ambapo mshindi wa kwanza alikuwa
Tamasha Mkwechi amezawadiwa fedha taslimu elfu thelathini,Agripina Pweleza elfu
25 na Emili Mgabe shilingi elfu 15 na kikundi kimepata baiskeli aina ya foneksi
na shilingi elfu 50.
Aidha akizungumza kwa niaba ya wakulima wa shamba Darasa
katika Kitongoji cha Manyomvi Bi Tamasha Pweleza amesema kuwa wanaushukuru
mradi wa Mkuhumi kwa kutoa mafunzo hayo na kwamba wananchi wameweza kufuatilia kwa kina na wameiomba
serikali itoe mikopo ya pembejeo kwa wakulima hao ili waweze kuendeleza kilimo.
No comments:
Post a Comment