Saturday, December 11, 2010

WANYANG'ANYWA ARDHI YAO HUKO BABATI BILA YA KUPATIWA FIDIA YOYOTE.



WAADHIMIA KUFANYA MAANDAMANO BAADA YA KUNYANG'ANYWA ARDHI YAO BILA FIDIA BABATI
.


BAADHI ya wakazi wa mtaa wa Bagara ziwani wilayani Babati wameazimia kufanya maandamano ya amani hadi kwa Mkuu wa mkoa wa Manyara,Henry Shekifu kutokana na kilio chao cha muda mrefu cha kunyang'anywa ardhi yao bila fidia ya maana.

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi mjini Babati huku wakiwa na masikitiko makubwa wakazi hao zaidi ya 48 walidai kuwa wataandamana hadi kwa Mkuu huyo wa Mkoa na endapo kilio chao hakitasikilizwa watakwenda kulalamika kwa waziri mwenye dhamana ya ardhi.

Mmoja kati ya wakazi hao Athumani Omary alisema kuwa wamemiliki ardhi hiyo kwa zaidi ya miaka 40 lakini serikali inataka kuwahamisha bila kuwafidia na kuwapa eneo jingine.

Omary alisema katika ardhi hiyo yapo makaburi ya wazazi wao waliofariki na kuzikwa hapo pia kuna watu waliozaliwa kwenye ardhi hiyo hivyo hawatakubali waporwe ardhi yao kwa urahisi.

Naye Sakwara Muna alisema japo Babati ni makao makuu ya mkoa wa Manyara hawapingi eneo lao kutumika kwa ajili ya kupatikana maendeleo lakini wanapaswa wapatiwe eneo mbadala la kuhamia.

Muna alisema kama Serikali imeamua eneo la Bagara ziwani ni la kujengea majengo mapya ya taasisi mbalimbali za kibinafsi na serikali inatakiwa kuwajali wale wanaoishi kwenye eneo hilo.

Mkazi mwingine Tatu Sakwara alisema baadhi ya viongozi wa ardhi wilayani Babati wamekuwa wakitoa fidia ambayo hailingani na thamani ya ardhi kwani familia yenye makaburi na ardhi ya eka 10 huwezi kuwapa sh 200,000 kwa kila eka.

Sakwara alisema kuwa hivi karibuni Jeshi la polisi mkoani humo lilijenga makazi ya polisi baada ya kununua eneo kwa sh 78 milioni lakini hawajaambulia chochote kwenye fedha hizo.

Hata hivyo Mwenyekiti wa mtaa huo,Juma Akedai alikiri kufahamu mgogoro huo na kudai kuwa wakazi hao wananyanyaswa kutokana na kutotendewa haki na Serikali.

No comments:

Post a Comment