Tuesday, June 10, 2014

MAMIA YA WAKAZI WA MOROGORO WAHUDHURIA KESI YA MTOTO NASRA ALIYEFARIKI DUNIA HIVI KARIBUNI





Kesi inayowakabili walezi wa Marehemu Nasra Rashid Mvungi ya kuhusika na unyanyasaji pamoja na mateso ya kumfungia mtoto huyo kwenye box kwa muda wa miaka mitatu na nusu, imesikilizwa tena kwa mara ya pili katika mahakama ya Mkazi Morogoro na kuhahirishwa mpaka June 12 mwaka huu kutokana na washtakiwa hao kutakiwa kuhojiwa upya na jeshi la polisi.

Kesi hiyo iliyovutia hisia za wakazi wengi wa manispaa ya Morogoro imeketi chini ya Hakimu Mkazi mfawidhi Mary Moyo mapema asubuhi ya leo kwa ajili ya usikilizwaji wa awali huku washitakiwa akiwemo baba mzazi wa Marehemu Nasra, Rashidi Mvungi,na walezi wa mtoto huyo Mariamu Said,na Mtonga Omary wanashitakiwa kwa makosa mawili ya kula njama na kumfanyia ukatili wa kumtekelekeza na kumpa malezi akiwa ndani ya boksi kwa muda wa  miaka mitatu na kumsababishia maradhi ya mvunjiko wa mifupa katika mwili wake na kupelekea kifo chake.
Picha ya Mtoto Nasra enzi za Uhai wake
Katika kesi hiyo wakili wa serikali Sunday Hyera ameiomba mahakama ya hakimu mkazi Morogoro kusimamisha usikilizaji wa awali wa kesi hiyo,na kuomba kuhojiwa upya kwa washtaki  hao na jeshi la polisi mkoani hapa. 

Wakili wa serikali amesema  kutokana na mtoto Nasra kufariki anaiomba mahakama kutaja tarehe  ya karibu kwa ajili usikilizaji mwingine wa kesi hiyo, mara baada ya kukamilika kwa mahojiano na uchunguzi kwa watuhumiwa hao.

Mahakama chini ya hakimu wake Moyo amesema hakuna pingamizi kuhusiana na ombi hilo la washtakiwa kwenda kuhojiwa upya na kufanyiwa uchunguzi, ambapo washtakiwa hao wametakiwa kurudishwa rumande mpaka hapo kesi hiyo itakaposikilizwa tena June 12 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment