Wednesday, June 18, 2014

WAZAZI WILAYANI KILOSA WAPIGWA MARUFUKU KUWATUMIKISHA WATOTO



Mkuu wa wilaya ya Kilosa Elias Tarimo amepiga marufuku wanafunzi kujishughulisha na biashara yoyote pindi wawapo shuleni na nyumbani ili kutimiza Sera ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto.
                                watatu kutoka kushoto ni mkuu wa wilaya ya kilosa elias Tarimo
Tarimo ameyasema hayo Juni 16 mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika Kiwilaya katika Kata ya Zombo  kijiji cha Nyali na kusema kuwa ni marufuku kwa wazazi kuwatuma watoto kufanya biashara yoyote ile kwani ni kinyume na sheria.
Pia amesema kuwa tabia ya kuwaajiri watoto  katika shughuli mbalimbali ni kosa hivyo Halmashauri ya Wilaya Kilosa wanatengeneza sheria ya kupinga watoto kufanyishwa kazi kwani inawasababishia kuwa watoro mashuleni na kutokufanya vizuri darasani kwa kuwaza kufanya biashara hizo.
                             watoto wakiwa katika sherehe za kusherekea siku ya mtoto wa Afrika katika kijiji cha nyali wilayani kilosa mkoani morogoro
Aidha Tarimo amesema kuwa wazazi wanawajibu wa kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji yote muhimu shuleni kama vile madaftari na sare za shule ili kujenga mazingira rafiki ya kusoma na kujifunza ili kutekeleza mpango wa Serikali wa matokeo Makubwa Sasa(B.R.N) kwani Elimu ndiyo chachu ya Maendeleo.
                                Taarifa ya Camfed wa kuhusiana na huduma zao kwa watoto
Sambamba na hayo amewaasa wazazi kuwapeleka watoto shule kwa kipindi muafaka na kuhakikisha mtoto anakuwa shuleni muda wote wa masomo kwani kila mtoto ana haki ya kupata Elimu bila kujali jinsia wala ulemavu.

No comments:

Post a Comment