Monday, March 4, 2013

PONGEZI KWA AZAM FC KUSONGA MBELE


Release No. 037
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Machi 4, 2013

PONGEZI KWA AZAM KUSONGA MBELE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani katika michuano hiyo ya Afrika.

Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi inayofuata.

Timu ya Azam inayofundishwa na Mwingereza John Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na jana kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.

Kwa kufanikiwa kuing’oa Al Nasir Juba, Azam sasa watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya michuano dhidi ya Barrack Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha suluhu katika mechi ya marudiano jijini Freetown.

Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi 15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment