Tuesday, March 12, 2013

WANAFUNZI WILAYANI KILOMBERO WAHIMIZWA KUONGEZA BIDII KATIKA MASOMO YAO KUEPUKA AIBU YA MATOKEO KATIKA MITIHANI YAO YA KUHITIMU

WANAFUNZI WILAYANI KILOMBERO WAHIMIZWA KUONGEZA BIDII KATIKA MASOMO YAO

Wanafunzi wilayani Kilombero wamehimizwa kuongeza bidii katika masomo ili wafanye  vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne na kuondokana na aibu ambayo taifa imepata  kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne  kwa mwaka 2012 kufeli.

Hayo yameelezwa leo na mbunge wa jimbo la Kilombero Mheshimiwa Abdul Mteketa wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kata ya Kibaoni alipokuwa akitoa msaada wa vitabu 100 vya masomo ya hesabu,jiografia,kemia,fizikia na bailojia katika shule hiyo.

Mh,Mteketa amesema kuwa kufeli kwa wanafunzi wengi inatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vitabu ,walimu na baadhi ya wanafunzi kutokuwa na nidhamu hivyo amewataka   wazazi ,walezi na walimu kushirikiana  kikamilifu ili kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo .

Kuhusu baadhi ya wanafunzi kutokuwa na nidhamu kwa walimu na utoro,amesema suala la nidhamu kwa mwanafunzi ni ushirikiano kati ya wazazi na walimu na hivyo amewataka wazazi kuwa wakali kwa watoto wao pindi wanapokosea  badala ya kuwatetea , hali hiyo inasababisha wanafunzi wengi kutokuwa na nidhamu pindi wanapoona wanatetewa na wazazi wao.

Awali akizungumza wakati akipokea msaada huo kwa niaba ya shule mkuu wa shule hiyo  Bwana Zakaria Kalinga amemshukuru Mh Mteketa  kwa msaada wa vitabu 100 na amemuomba asichoke kuitembelea shule hiyo na kutatua changamoto zinazowakabili ili kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo.

Bwana Kalinga amesema shle hiyo inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vitabu,uchache wa samani za ofisi,uhaba wa walimu hasa wa masomo ya sayansi,ukosefu wa nyumba za walimu,ukosefu wa hostel na ukosefu wa vifaa vya michezo na fedha kwa ajili ya matengenezo ya uwanja .

Kuhusu vifaa vya michezo na matengenezo ya uwanja mbunge huyo  amewaahidi atahakikisha anatekeleza ahadi hiyo.

No comments:

Post a Comment