Thursday, March 7, 2013

SERIKALI YA KIJIJI CHA MCHOMBE YAHUSIKA NA UPOTEVU WA FEDHA JUMLA YA MILIONI 2.19

WANANCHI WA KIJIJI CHA MCHOMBE WAWAONDOA VIONGOZI WAO  WA SERIKALI MADARAKANI.


Wananchi wa Kijiji cha Mchombe wamewaondoa madarakani viongozi wa serikali ya kijiji hicho  katika mkutano wa kijiji kutokana na kuhusika na upotevu wa fedha jumla ya shilingi 2,190,000.

Kaimu Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mngeta Bwana Shabani Mgaya amesema kuwa Kuondolewa madarakani kwa serikali hiyo kumetokana na taarifa ya mkaguzi wa ndani wa hesabu za serikali kubaini  makosa mbalimbali yaliyofanywa na serikali hiyo.

Amesema serikali hiyo imefanya upotevu wa shilingi 2,190,000 ambazo zimepotea kwa uzembe wa viongozi hao ambapo shilingi 1,780,000 ilitolewa benki na ilitumika bila ya idhini ya serikali.

Aidha Bwana Mgaya amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi imeeleza kuwa kati ya fedha hizo shilingi 300,000  zilitokana na uuzwaji wa ardhi ya kijiji ambapo ni kinyume na sheria kwani ardhi hiyo iliuzwa bila ya kufuata taratibu na pesa hiyo haikuonekana.

 Taarifa hiyo ya mkaguzi ambayo imewafanya wananchi kuuondoa uongozi madarakani imeeleza kuwa shilingi 1,100,000 fedha kutoka mfuko wa jimbo ambayo ilikuwa kwa ajili ya uchimbaji wa visima imetumika kwa matumizi mengine tofauti na yaliyokusudiwa.

 Aidha miongoni mwa mambo yaliyobainika katika taarifa ya  mkaguzi wa ndani kwa viongozi wa serikali hiyo ni udhaifu wa serikali katika kukusanya mapato,udhaifu wa kutosimamia shughuli za maendeleo na kutosoma taarifa za mapato na matumizi kwa vipindi vitatu mfululizo.




No comments:

Post a Comment