Wednesday, June 18, 2014

WATOTO 863 WAMERIPOTIWA KUFANYIWA VITENDO VYA KULAWITIWA

Imeelezwa kuwa jumla ya watoto 863 wameripotiwa kufanyiwa vitendo vya ulawiti huku wanaowafanyia hivyo wakiwemo ndugu zao wa karibu na  watoto 250 wametupwa na kutelekezwa ambapo 142 wakiwa wametekwa na watoto 10 wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji.
Hayo yameelezwa Jijini Dar es salaam juni 16 mwaka huu na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC)  Harold Sungusia wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika na kuelezea changamoto mbalimbali zinazo wakabili watoto.
Sungusia amesema kuwa kutokana na kukithiri kwa hali hiyo ya ukatili dhidi ya watoto, ametaka Haki na Ulinzi wa watoto iwe ajenda ya kila mdau hasa Wanasiasa kuifanya kitaifa katika mikutano yao.
Ameongeza kwa kusema kuwa wanasiasa wanapaswa kufanya hivyo wakiamini kwamba itahamasisha wananchi kwa uzito mkubwa kutokana wao kuwa na nafasi kubwa ya kusikilizwa na kuwafikia wananchi wengine kwa wakati.
Pia ameitaka Serikali iweke mikakati  ya kiulinzi itakayo muwezesha mtoto kujitambua na kujilinda mwenyewe kabla ya mtu mwingine  na kuongeza kuwa wananchi  kwa ujumla wanapaswa kuheshimu nafasi ya watoto katika jamii na pale ambapo Haki zao zinakiukwa basi ni vizuri kutoa taarifa katika sehemu husika.

No comments:

Post a Comment